MAKALA


HIJABU YA MWANAMKE WA KIISLAM

KATIKA QUR-AN NA SUNNA 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma na mwenye kurehemu. Kila sifa njema na shukrani zote anastahiki Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote. Sala na amani ziwe juu ya ya mja wake na Mtume wake Nabii Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambae ametumwa kuwa mwalimu na rehma kwa walimwengu wote.

 

Namshukuru Allah kwa kunijaalia kuandika makala hii ya Hijabu ya Mwanamke wa Kiislam na kuiwasilisha kwa jamii katika tovuti hii ya Mwanamke wa Kiislam.

 

Ni kweli na ni hakika kwamba inasikitisha sana kwa wanawake mbali mbali wa Kiislam kwa namna ya mavazi wanayovaa kila siku zinavyokwenda, aiku hizi wanawake wengi wamekuwa wakivaa mavazi yasiyo na stara, wanavaa mavazi ya kikafiri, ambapo ukiwaangalia utaona kuwa hakuna tofauti baina yao na Mayahudi au hata Wakristo, na hali hii imekuwa ni hatari kubwa sana katika maisha ya Uislam, na kupelekea au kusababisha kushuka kwa hasira ya Mwenyezi Mungu na yakateremka maangamizo na kuangamia wema na wabaya.

 

Na lengo ni wale mawalii amri wa hao wanawake wanawaachia wake zao na mabinti zao na dadfa zao kuvaa nguo za kikafiri na kutoka nje ya nyumba zao bila ya kuvaa baibui na hijaab. Na yakizodi mambo haya ni sababu ya kushuka maangamizo kutoka mbinguni na kuwaangamiza wote wabaya na wema.

 

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Anfaal aya ya 25 amesema:-

 

“NA IOGOPENI ADHABU YA MWENYEZI MUNGU HAPA DUNIANI AMBAYO HAITAWASIBU PWKW YAO WALE WALIODHULUMU NAFSI ZAO MIONGONI MWENU BALI ITAWASIBU HATA WALIONYAMAZA WASIYAKATAZE MAOVU. NA WENGINEO PIA. NA JUENI YA KWAMBA MWENYEZI MUNGU NI MKALI WA KUADHIBU.”

 

Kutokana na ukali wa aya hiyo ya Mwenyezi Mungu enyi Mawalii amri wakatazeni wake zenu mabinti zenu na dada zenu, na waamrisheni waisitiri miili yao, na iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu, la si hivyo mtasababisha kuwashukia hasira ya Mwenyezi Mungu kwa wote.

 

Uislam ni Dini iliyoleta sheria na adabu za Kiislam, na baadhi yake ni sheria ya vazi la Kiislam kwa wanawake wa Kiislam.

 

Wanawake wa kiislam wamekuwa na tabia mbaya iliyo kinyume na maamrisho ya dini yao kwa kwenda makazini kukaa mabarazani au hata kupita katika masoko wakiwa uchi, wanaonesha miili yao ovyo kwa wanaume wanaoweza kuwaoa (Ajnabi) bila hata kuwa na hofu juu ya Mola wao au hata kuona haya ama aibu ya aina yeyete ile. Na tabia hii ni katika mambo mabaya sana na ni hatari kubwa sana katika jamii ya Kiislam kwa haya maasi makubwa kabisa yanayofanywa na wanawake ikiwa ni dada zetu mama zetu wake zetu au hata mabinti zetu na hata wa wenzetu.

 

Hijaab ya mwanamke wa Kiislam imekuja kwa malengo maalum kama sheria ya kustiri miili ya wanawake, kwa kuamrishwa wanawake wa Kiislam kuisitiri miili yao kwani kufanya hivyo ni salama kwao na ni kuepukana na Shetani kwa kufanya mambo machafu na mengine yaliyokuwa mabaya na yenye kuvutia matamanio mabaya.

 

Sharia ni lazima kwa kila walii, ambao ni wazazi, au waume au kaka au ndugu, na wanatakiwa wasinyamaze na kuwaregezea watu wao wa kike kutoka katika misingi ya sheria na adabu ya Kiislam.

 

Tabia hii ya kuwaachia wanawake inawapasa (wanaume) au hata wanawake kuikataza jamii nzima ya wanawake wa Kiislam na wasiachiwe kabisa kuvaa mavazi ya kikafiri na kutoka nayo nje bila ya kusitiri miili yao.

 

Faradhi hii ni ya kila Muislam ya kuamrisha mema na kukataza mabaya, kwani kunyamaza kimya bila ya kukataza mabaya ni sababu kubwa ya kutyokea maafa mbali mbali katika jamii ya Waislam na hatimae kufikwa na maangamizo.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“HAKIKA WATU WANAPOONA MABAYA YANAFANYIKA KISHA WASIYABADILI KWA KUYAKATAZA, WAKANYAMAZA NA KUPUUZA BASI IMEKARIBIA KUWASHUKIA ADHABU YA MWENYEZI MUNGU”

 

Na katika Qur-an Mwenyezi Mungu Mtukufu sehemu nyingi amesimulia habari za maangamizo waliyoangamizwa watu wa Israil kutokana na kutokataza mabaya, walikuwa wanaona mabaya yanafanyika laini walibyamaza kimya bila ya kukatazana, na hapo ndipo ilipowashukia laana na adhabu ya Mwenyezi Mungu juu yao kutokana na kunyamaza kimya kwao.

 

Katika Surat Al-Maaida aya ya 78/79 Mwenyezi Mungu amesema:-

 

“WALILAANIWA WALE WALIOKUFURU MIONGONI MWA WANA WA ISRAIL KWA ULIMI WA NABII DAUD NA NABII ISSA IBN MARYAM. HAYO NI KWA SABABU WALIASI NA WAKIRUKA MIPAKA YA MWENYEZI MUNGU. HAWAKUWA WENYE KUKATAZANA MAMBO MABAYA WALIYOKUWA WAKIYAFANYA, MAOVU YALIOJE YA MAMBO HAYO MABAYA WALIYOKUWA WAKIYAFANYA.”

 

Hiyo ndiyo hatari ya kuyaona mabaya yanafanywa kasha watu wakanyamaza kimya bila hata kuyakataza.

 

Sasa hao mawalii (wazee ikiwa ni wanaume au hata wanawake) wa kina dada, wake au mabinti ndio waliolazimika kuyasimamia na kuwakataza wanawake kuvaa mavazi ya kikafiri sio kuregeza na kunyamaza kimya.

 

Lakini utakuta hao mawalii wenyewe wamenyamaza, na kunyamaza kwao ina maanishwa kuwa wako radhi kuwaachia watoto wao, wake zao, dada zao au hata mama zao kuonesha miili yao kwa watu ajnabi. Na hii ndio sababu ya kushuka hasira na adhabu za Mwenyezi Mungu wakaangamia wema na wabaya kutokana kunyamaza kwa kutoyakataza mabaya.

 

Basi hapo laana ya Mwenyezi Mungu humpata kila mtu. Na ni sababu za maangamizo zinakuwa namana hiyo za kutokataza mabaya na kunyamaza kimya.

 

Na hao mawalii wananyamaza na kuwaachia wake zao na dada zao na watoto wao kuvaa nguo za kubana na kutoka nje bila ya kuvaa hata baibui, wanaonesha miili yao ovyo huko nje. Kila mtru ajnabi huko nje anausoma mwili wa mwanamke ulivyo, na hali huyo mwanamke ni Muislam.

 

Tujiulize je huyo tutamwita kuwa ni mwanamke wa Kiislam? Kichwa chake kiwazi na ikiwa kajitanda basi huo mtandio si wa sitara, bali mtandio wa pambo tu, kichwa chote kinaonekana. Au atafunika kichwa vizuri kwa huo mtandio au ushungi lakini, lakini kava nguo za kubana, mwili wake wote unaonekana, unamuona viumgo vyote vya mwili wake, jee! Huyo tuamwita mwanamke wa Kiislam?

 

Mwanamke wa namna hiyo yeye na kafiri ni sawa kabisa, hana Uislam wowote, na hali ya kuwa Uislam umeleta sheria ya vazi la wanawake wastiri miili yao.

 

Mwenyezi Mungu Mtukufu alipokuwa akiwahutubia wake wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  ambapo hotuba inayowahusu wake wa mtume ni kwa ajili ya Waislam wote.

Amesema katika Surat Al Ahzab aya ya 33:-   

 

“NA KAENI MAJUMBANI MWENU WALA MSIONESHE MAPAMBO YA MIILI YENU KAMA WALIVYOKUWA WAKIONESHA MAPAMBO YAO WANAWAKE WA ZAMA ZA UJAHILIYA.”

 

Wafasiri wa aya hii wamesema maana ya “TABARRUJIL-JAAHILIYYAH” Ya kuwa ni kuonesha mwanamke namna ya pambo la mwili wake ulivyo ili avutike mwanamme aingiwe na matamanio mabaya ya zanaa.

 

Katika zama za ujahiliya mwanamke alikuwa anajitahidi  kuupamba mwili wake na kuvaa nguo za kubana na nyepesi ili mwili wake uonekane vizuri na wanaume, basi mwanamme yeyote tule akimuona tu mwanamke alievaa nguo za kubana namna hiyo akauona mwili wa mwanamke huyo, hupiga katika moyo wake tamanio baya unamsadikisha na kuingia katika maovu ya kuzini. Hivi ndivyo walivyotafsiri wataalam juu ya maana ya “TABARRUJIL-JAAHILIYYAH” Ni kwamba kuonesha pamno la mwili wake mwanamke ili avutike mwanamme kwa tamanio la zinaa.

 

Vile vile maana ya “TABARRUJIL-JAAHILIYYAH” imetafsiriwa kuwa ni kuonesha mwili wake mwanamke na kutembe utembezji wa kudeka na kulainika mwili wake na kuilegeza miguu yake katika mwendo wake wa kuilegeza shingo yake ili kichwa chake kilegee kwa kunyongeka na kulainika kama ilivyolainika nundu ya ngamia, maana wale ngami walionona wakitembea nundu zao hulainika na hunama mara kulia na mara kushoto.

 

Basi wanawake waliotajwa kuhusu “TABARRUJIL-JAAHILIYYAH” ndio vichwa vyao sawa na hizo nundu za ngamia, na kuvaa nguo ambazo si za stara.

 

Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“WANAWAKE WAMEVAA MAVAZI YA UCHI (YAANI NGUO SI ZA STARA) WAMEELEMEA KUINAMA (KUPENDA MAVAZI YASIYOKUWA YA STARA), VICHWA VYAO KAMA NUNDU ZA NGAMIA VIMEINAMA HAWATAINGIA PEPONI WALA HAWATAPATA (HATA) HARUFU YAKE (PEPO).”

 

Ndio nguo wanazovaa wanawake siku hizi za kukaa uchi tu, si nguo za stara, bali nguo za mapambo ya kuonesha miili yao, ambazo alizozitaja Mtume  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Na Mwenyezi Mungu kabainisha namna ya nguo za Kiislam na sheria kwa mwanamke wa Kiislam amelazimisghwa avae kwa ajili ya kusitiri mwili wake. Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awaambie wanawake wa Kiislam katika Surat Nuur aya ya 31:-

 

“NA (EWE NABII MUHAMMAD) WAAMBIE WAISLAM WANAWAKE WAINAMISHE MACHO YAO, NA WAZILINDE TUPU ZAO WALA WASIDHIHIRISHE VIUNGO VYAO VYA MWILI KWA WATU ISIPOKUWA VINAVYODHIHIRIKA KAMA USO NA VIGANJA VYA MIKONO, NA WAANGUSHE SHUNGI ZAO AU MITANDIO MPAKA VIFUANI MWAO, NA WASIONESHE MAPAMBO YAO ILA KWA WAUME Z\AO, AU BABA ZAO, AU BABA ZA WAUME ZAO, AU WATOTO WAO, AU WATOTO WA WAUME ZAO, AU KAKA ZAO, AU WATOTO WA KAKA ZAO, AU WATOTO WA DADA ZAO, AU WANAWAKE WENZAO, AU WALE ILIYOMILIKI MIKONO YAO YA KUUME, (YAANI WATUMWA WAO) AU WAFUASI WA WANAUME WASIOKUWA NA MATAMANIO YA WANAWAKE, AU WATOTO AMBAO HAWAJAJUA MAMBO YANAYOHUSU UKE, WALA WASIPIGE MIGUU YAO ILI YAJULIKANE WANAYOYAFICHA KATIKA MAPAMBO YAO. NA TUBIENI NYOTE KWA MWENYEZI MUNGU, ENYI WAISLAM ILI MPATE KUFUZU.”

 

Sasa hiyo ni amri ya Mwenyezi Mungu anakataza wanawake kuonesha miili yao, waisitiri kweli kweli, sio kuiweka wazi miili yao ikawa inaonekana na watu ovyo. Jee huo ndio Uislam? Ukweli ni kwamba huo si Uislam kabisa huko ni kwenda kinyume na sheria za Mwenyezi Mungu.

 

Wanaamrishwa wanawake waisitiri miili yao, pamoja na kuinamisha macho yao wanapopita mbele za watu, wasipepese macho kutazama watu. Kama walivyoamrishwa wanawake wainamishe macho yao basi pia hata wanaume wameamrishwa wainamishe macho yao wanapopita mbele ya wanawake, wasipepese macho yao kutazama wanawake, na amri hiyo pia ni katika Surat Nuur katika aya ya 30:-

 

“SEMA (EWE NABII MUHAMMAD) UWAAMBIE WAISLAM WANAUME WAINAMISHE MACHO YAO (WASITAZAME WANAWAKE AU YALIYOKATAZWA), NA WAZILINDE TUPU ZAO, (ILI WASIINGIWE NA MATAMANIO MABAYA), KUFANYA HIVYO NI TAKASO KWAO (WANATAKASIKA NA KUEPUKANA NA MARADHI YA MACHAFU YA ZINAA.)”

 

Kwa sababu mwanamme akimtazama mwanamke siejietiri mwili wake, viungo vya mwili vyote vinaonekana, basi mwanamme huingiwa na tamanio baya la zinaa, na hiyo ndio hatari yenyewe. Na wanawake wasiositiri miili yao, basi wanawasababishiwa wanaume kupata madhambi.

 

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):-

 

“MWENYE KUTAZAMA UZURI WA MWANAMKE AJNABI KWA MATAMANIO (MACHAFU YA ZINAA, BASI) HUMWAGIWA MACHONI MWAKE RISASI ILIYOYEYUSHWA KWA (MOTO) SIKU YA KIAMA.”

 

Kwa hivyo sasa hatari ya manaume inawata kwa sababu ya wanawake wasiojistiri miili yao. Hii ndio sababu Mwenyezi Mungu anaamrisha kwa wanaume na wanawake kuinamisha macho yao ili wasalimike na mambo yanayovutia machafu ya zinaa.

 

Lakini mwanamke ikiwa hakuustiri kwa kuuficha mwili wake kwa nguo za stara kama ilivyoamrishwa na sheria ya Uislam, jee mwanamme ataweza kuinamisha macho yake? Kwa kuwa mwanamke kava nguo za kubana, na mwili wake wote unaonekana ulivyo, viungo vyote unaweza kuvihesabu na kuviona vilivyo, ina maanisha umbo lake lote unaliona alivyoumbwa, hakuna tofauti yoyote na aliyekaa uchi. Jee! Huyo mwanamke kaustiri mwili wake? Huyo si yuko uchi tu.

 

Sasa mwanamme akiona mwanamke alievaa vazi hilo ataweza kuinamisha macho yake? Kwa sababu kuna wanaume wengine wana maradhi ya tabia chafu, na anataka tu na kupenda atazame mambo kama hayo. Baada ya kuinamisha macho yake, basi ndio atazidi kuinua macho yake na kuyafungua zaidi ili aone kiroja cha mwili wa huyo mwanamke.

 

Na hapo sasa ndio Shetani anaingia baina yao, yule mwanamme moyo wake unamuanguka, na utupu wake unamsadikisha kwa matamanio machafu ya zinaa. Na hapo sasa yule mwanamke atakuwa kishazini na yule mwanamme aliyouona mwili wa yule mwanamke, ijapokuwa hawakulala kitanda kimoja.

 

Na yule mwanamke anakuwa katika hukumu ya kuzini, na anapata dhambi za kuzini, na kuwa na hukumu ya janaba katika mwili wake. Na lazima kwanza aende akakoge ukogakji wa janaba, na haimjuzii kusali wala kufanya ibada yoyote, kwa ajili ya kuweka mwili wake wazi ukaonekana na watu ajnabi, kwani macho nayo yanazini.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“KILA JICHO LIMEZINI”   

 

Ina maanisha kuwa kila jicho la mtu aliyemtazama yule mwanamke basi kazini na yule mwanamke aliyekuwa hajajistiri mwili wake kwa kuuacha mwili wake waziukaonekana na wanaume ajnabi.

 

Kwa hivyo mwanamke wa aina hiyo asiejistiri mwili wake, basi tangu ametoka nyumba kwake katika safari zake mpaka mpaka anarudi nyumbani kwake au kwao, jee jiulize ni macho mangapi ya watu yaliyomtazama huyo mwanamke? Ikiwa ni watu kumi au elfu, basi wote hao amezini nao, na anapata madhambi ya kuzini na watu wote hao waliouona mwili wake.

 

Na hiyo ndiyo  “TABARRUJIL-JAAHILIYYAH”  iliyotajwa katika Surat Al-Ahzab tuliyoifasiri hapo nyuma. Na hali Mwenyezi Mungu kawakataza wanawake wa Kiislam waache kabisa wasifanye hayo mambo ya kijahiliya. Na leo wanawake wa Kiislam wanaurejesha wenyewe ujahiliya na wanakanusha amtri ya Mwenyezi Mungu aliyoamrisha waistiri miili yao wanawake wa Kiislam.

 

Jee hiyo si hatari kunwa kabisa? Basi mwanamke wa namna hiyo kila siku anapata mambo haya yafuatayo:-

(a). Anapata laana ya Mwenyezi Mungu na hasira yake, na analaaniwa na kila anaelaani.

(b). Anapata dhambi za kuzini.

(c). Daima anakuwa katika hukumu ya mwili mchafu wa janaba.

(d). Sala yake wala ibada yake yoyote haikubaliwi, wala haipandishwi amali yake mbinguni hata shibiri moja.

(d). Hukumu yake anakuwa katika idadio ya miongoni mwa mkafiri, na wala si Muislam tena unamtoka Uislam kabisa.

 

Na mwanamke wa aina hiyo asiekuwa na haya wala kumuogopa Mola wake, basi huyo ni kafiri tu. Maana tabia ya dini ya Kiislam basi mtu ni kuwa na haya.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“NA KILA DINI INA TABIA, NA TABIA YA DINI YA UISLAM (MTU KUWA NA) HAYA (AIBU).”

 

Na mwanamke aneuonesha mwili wake wote mabarabarani na katika afisi za kazi na hadi katika masoko bila ya kuona haya wala kumuogopa Mola wake. Hajali kabisa hayo, anapita barabarani kichwa wazi, au kafunika kichwa lakini mwili wake wote uko wazi na kava nguo za kubana, au nguo fupi. Hiyo ndiyo “TABARRUJIL-JAAHILIYYAH”  . Yeye na kafiri hawana tofauti.

 

Au tukitazama katika Surat Al-Ahzab tunaona Mwenyezi Mungu anaamrishwa zaidi wanawake waisitiri miili yao, maana kustiri miili yao basi ni salama yao wenyewe, na wanaepukana na na udhia kutokana na watu wenye tabia mbaya. Mwenyezi Mungu katika Surat Al-Ahzab aya ya 59 amesema:-

 

“EWE NABII (MUHAMMAD)! WAAMBIE WAKE ZAKO, NA MABINTI ZAKO, NA WANAWAKE WA WAISLAM (YA KWAMBA) WAZITEREMSHE NGUO ZAO (KWA KUSTIRI MIILI YAO,) KUIFANYA HIVYO NI KUWAPELEKA UPESI WAJULIKANE (YA KWAMBA WAO NI WANAWAKE WENYE HESHIMA) ILI WASIUDHIWE NA WATU (WENBYE TABIA MBAYA), NA MWEYEZI MUNGU NI MWINGI WA KUSAMEHE NA MWINGI WA KUREHEMU.”

 

Sasa hapa Mwenyezi Mungu anaamrisha wanawake wa Kiislam wazidi kuisitiri miili yao. Maana miili ya wanawake kuiweka wazi ikaonekana na wanaume ajnabi ndio sababu kubwa kwa Shetani kuvutia mambo machafu ya zinaa. Na wanawake ndio fitna (ina maana kuwa) mtihani mkubwa sana kwa wanaume kufanya mambo machafu ya zinaa.  

 

Mwenyezi Mungu katika Surat Al-Imraan aya ya 14 amesema:-

 

“WAMEPAMBIWA WATU (KUTILIWA) HUBA YA KUPENDA STAREHE YA WANAWAKE……….”

 

Ina maanisha kwamba Mwenyezi Mungu amewaumba watu na kasha akawatilia (element) tabia ya kupenda matamanio ya starehe ya kimwili ya wanawake, ili awafanyie mtihani waja wake kwa mambo haya.

 

Ukisoma katika “ASILI YA UONGOFU” Juzuu ya pili, tafsiri ya Surat Aal-Imraan aya hii ya 14 utaona yametajwa mambo mengi sana juu ya hatari hii ya mtihani wa kupenda matamanio ya wanawake.

 

Na ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:-

 

“SIKUACHA (NYUMA) BAADA YANGU FITNA (YAANI MTIHANI) WENYE MADHARA MAKUBWA KABISA JUU YA WANAUME (KAMA MTIHANI WA MATAMANIO YA) WANAWAKE.”

 

Na wanawake ndio mtihani mkubwa sana alioufanya Mwenyezi Mungu kwa binaadamu. Hao wana wa Israil hapo zamani yaliwapata maangamizo mengi sana, na sababu ya maamizo hayo ni wanawake.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“NA IOGOPENI DUNIA, NA WAOGOPENI WANAWAKE, BASI KWA HAKLIKA MTIHANI WA MWANZO (WA KUANGAMIZWA) WANA WA ISRAIL ULIKUWA (KWA AJILI YA MAMBO MACHAFU YA) WANAWAKE.”

 

Na vile vile tumeshazitaja zile aya mbili za 78 na 79 katika Surat Maaida, (tazama). Basi hasira na ghadhabu za Mwenyezi Mungu huteremka ikashuka adhabu na maangamizo yake kwa watu, basi sababu ya mwanzo inakuwa ni wanawake kuonesha miili yao ovyo kwa wanaume ajnabi ikawa sababu ya kutapakaa machafu ya zinaa.

 

Na Uislam unakataza kabisa kuchanganyika wanaume na wanawake pamoja. Inatakiwa mwanamme ajnabi asimuone mwanamke ajnabi, au mwanamke ajnabi asimuone mwanmme ajnabi, ila kwa dharura iliyoruhusu sheria ya Kiislam.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“ASISAFIRI MWANAMKE (PEKE YAKE) ILA PAMOJA NAYE AWE MUHRIM (WAKE), WALA ASIKAE MWANAMME KWA MWANAMKE PEKE YAO ILA PAMOJA NAYE AWEPO MUHRIM (WAKE.)”

 

Na akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):-

 

“WASIKAE PEKE YAO MWANAMME NA MWANAMKE ILA SHETANI ANAKUWA WATATU WAO.”

 

 

Na akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):-

 

“ASILALE MWANAMME (AJNABI) KWA MWANAMKE (KATIKA NYMBA PEKE YAO ILA AWEPO MUME (WAKE) AU MUHRIM (WAKE).”

 

Na akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):-

 

“SI HALALI (HAIMJUZII) MWANAMKE MWENYE KUAMINI MWENYEZI MUNGU NA SIKU YA KIAMA ASAFIRI MWENDO WA SIKU MOJA NA USIKU ISIPOKUWA AWE PAMOJA NAYE MUHRIM WAKE.”

 

Hapa itabidi tuweke waze kwa wale wasiojuwa maana ya “MUHRIM” na “AJNABI” kwa vile maneno haya ni ya Kiarabu. Hivyo ni bora kuweka wazi tafsiri zake kwa kuwa wengine watakuwa hawajui.

 

Neno “MUHRIM” lina maana mtu anayemuhusu wa damu ambae hawezi kumuoa huyo mwanamke. Mfano kama baba au ammi (ndugu wa baba) au mtoto au hata kaka,ndugu au mjomba na yeyote yule ambae hawezi kumuoa huyo mwanamke kama mama khaloo (mama mdogo au mkubwa) au binti, dada au shangazi na wengine ilimradi wasioweza kuoa. Hii ni maana na kusudio la neno “MUHRIM.”

 

Na neno “AJNABI”  Ni kwamba mwanamme yeyote au mwanamke yeyote, wanahusiana kwa damu au hawahusiani kwa jambo lolote, lakini wanaweza kuoana. Hiyo ndiyo maana ya  “AJNABI” ambayo yanatumika mara kwa mara katika makala hii.

 

Hivyo ikiwa wote wawili mwanamke na mwanamke ikiwa wao ni ajnabi basi haipaswi na haistahiki kabisa kuonana ovyo, au kuchanganyika pamoja wanawake na wanaume kwa ajili ya kuepukana na Shetani yasiwaingie matamanio mabaya ya zinaa. Ndio maana Uislam unakataza kabisa kuchanganyika wanawake na wanaume.

 

Na Mtume (S.A.W) alimuuliza binti yake Fatma (Radhiya Allaahu ‘anhu)  kasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Ewe Fatmah Nini imempasa mwanamke kuhusu mwanmme?

Akasema Fatma: Ewe Baba yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu! Imempasa mwanamke asionekane kabisa na mwanamme.

Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Umesema kweli ewe binti wangu! Kwa hakika umelelewa katika nyumba ya Nabii.

 

Na siku moja alikuja Asma bint Abu Bakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambae ni ndugu yake bibi Aisha (Radhiya Allaahu ‘anhu)  bint Abu Bakar, mke wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na Asma alikuwa kajipamba mapambo ya kike, mara akaja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuona Asma alivyojipamba, akamwambia Asma ya kwamba:-

 

“EWE ASMAA! HAKIKA MWANAMKE AKIFIKIA KUWA NA HEDHI (YAANI AKIBALEGHE) HAISIHI KWAKE (HAIMPASI) AONEKANE (NA MWANAMME AJNABI) ILA HIKI NA HIKI…AKAFANYA ISHARA MTUME (SWALLA ALLAAHU ‘ALAYHI WA AALIHI WA SALLAM) KATIKA USO WAKE NA VIGANJA VYA MIKONO YAKE.”

 

Na manna ya hadithi hii ni kwamba Mwanamke akisha baleghe tu, basi haijuzu kwake kuonesha mwili wake ila uso na viganja vya mikono tu. Ama sehemu yote ya mwili wake aisitiri kwa nguo zilizoamrisha sharia ya Kiislam.

 

Lakini leo wanawake wengi wa Kiislam wanakaa uchi tu kwa kuvaa hizo nguo fupi na za kubana, wanaonesha miili yao ovyo tu kwa watu ajnabi. Na Mwanamke wa Kiislam leo anapotaka kushonesha nguo, basi atakwenda kwa fundi amfungulie vitabu vyenye mitindo ya mishono ya mapambo na kubana ili aoneshe mwili wake vizuri huko nje kwa watu ajnabi.

 

Aoneshe pambo la kifua chake kilivyo, na vionekane viungo vya mwili wake vilivyo. Ilimradi ajitahidi achague ushoni wa kikafiri awe yeye na Myahudi na Mkristo na makafiri wengine sawa sawa, au kushinda huyo kafiri. Baadae yeye anasema kuwa ni mwanamke wa Kiislam, anasali na kufunga. Jee huyo mwanamke ana Uislam gani?

 

Huko ndiko kutabarruji Kujahiliya kwenyewe anashindana na amri za Mwenyezi Mungu. Na hali ya kuwa Mwenyezi Mungu amekataza kufanya hivyo?  Sasa mwanamke kama huyo vipi itapokelewa ibada yake? Na hali ya kuwa anakwenda kinyume na amri za Mwenyezi Mungu?

Haipandishwi juu ibada yake hta shibiri moja. Kajishabihisha yeye na Myahudi na Mkristo   na makafiri wengine sawa sawa, kaacha adabu na sheria za Kiislam na kufuata tabia za makafiri. Na anaejishabihisha  kuwa sawa na kufanana na watu basi yeye ni miongoni mwa watu hao aliofanana nao.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“MWENYEZI MUNGU AMEWALAANI WANAWAKE WENYE KUVAA NGUO ZA UCHI ZISIZOKUWA ZA STARA.”

 

Na Mwenyezi Mungu akimlaani kiumbe, basi kiumbe hicho kitalaaniwa na kila kitu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Baqra aya ya 159 amesema:-

 

“…… HAO NDIO ANAWALAANI MWENYEZI MUNGU, NA WANALAANIWA  (NA KILA) WENYE KULAANI.”

 

Basi mtu akilaaniwa na Mwenyezi Mungu, huyo pia analaaniwa na Malaika, Watu, Majini, Wanyama, Ndege, Wadudu, Samaki, Mbingu na Ardhi, Milima, Miti na viumbe vyote vyenye roho na visivyo na roho vinamlaani.

 

 

Basi na mwanamke wa Kiislam mwenye mwenye kuvaa nguo za kubana na kuonesha mwili wake, basi huyo analaaniwa na kila kitu, hata hiyo nguo anayoivaa inamlaani. Na anaelaaniwa na anaelaaniwa na Mwenyezi Mungu, basi huyo hatapata wa kumsaidia ila ni kuangamia tu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat An- Nisaa aya ya 52 amesema:-

 

“HAO NDIO MWENYEZI MUNGU AMEWALAANI, NA ANAELAANIWA NA MWENYEZI MUNGU BASI HATAPATA WA KUMNUSURU.”

 

Ina maanisha kuwa anaelaaniwa na Mwenyezi Mungu, basi huyo ni wa kuangamia tu, hatapata wa kumsaidia. Na yeyote anaemuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi huyo anasatahiki laana.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al- Ahzaab aya ya 57 amesema:-

 

“HAKIKA WALE AMBAO WANAMUUDHI MWENYEZI MUNGU NA MTUME WAKE, (BASI HAO) MWENYEZI MUNGU AMEWALAANI KATIKA DUNIA NA AKHERA, NA AMEWAANDALIA ADHABU IFEDHEHESHAYO (YA KUHINIKA).”

 

Na wanawake wenye kuvaa nguo za kubana zisizokuwa za stara wakaonesha miili yao ovyo watu ajnabi, basi hao ndio miongoni mwa waliomuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Basi hao inawapata laana ya Mwenyezi Mungu na kuwashukia ghadhabu zake.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Fat-h aya ya 6 amesema:-

 

“…… NA GHADHABU YA MWENYEZI MUNGU IKO JUU YAO NA KUWALAANI NA KUWAANDALIA (ADHABU YA MOTO WA) JAHANNAM, NAYO NI MAREJEO MABAYA KABISA.”

 

Na katika Surat Al- Imraan aya ya 87 amesema:-

 

“…… NA WANAFANYA UHARIBIFU KATIKA NCHI, HAO NDIO WATAKAOPATA LAANA, NA WATAPATA NYUMBA (YA MOTO WA JAHANNAM) ILIYO MBAYA KABISA.”

 

Na hao wanawake wenye kuvaa nguo za kubana na kuonesha miili yao watu ajnabi, basi hao ni miongoni mwa wanaofanya ufisadi na uharibifu katika nchi, na hali yamewafikia mawaidha ya Mwenyezi Mungu kuwakataza wasifanye hivyo kuonesha miili yao.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Baqra aya ya 89 amesema:-

 

“….. BASI YALIWAFIKIA YALE WALIYOKUWA WAKIYAJUA WALIYAKATAA, BASI LAANA YA MWENYEZI MUNGU IKO JUU YA MAKAFIRI.”

 

Na wanawake wenye kuvaa nguo za kikafiri na kuonesha miili yao watu ajnabi, yamewafikia mawaidha ya Mwenyezi Mungu na wanajua kuwa kuvaa nguo hizo kakataza Mwenyezi Mungu, na wao wanakanusha amri hii ya kustiri miili yao, basi wanakataa amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi laana ya Mwenyezi Mungu iko juu yao.

Na katika Surat Al- Ahzab aya ya 61 amesema:-

 

“(HAO) WAMELAANIWA POPOTE WANAPOKUWEPO…..”

 

Basi hao wanawake wasiostiri miili yao wanalaaniwa na Mwenyezi Mungu popote wanapokuwepo, na laana inawafuatia iko juu yao haikatiki duniani na akhera.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Qasas aya ya 42 amesema:-

 

“NA TUKAWAFUATISHIA LAANA (IKO JUU YAO) KATIKA DUNIA HII, NA SIKU YA KIYAMA WAO WATAKUWA MIONGONI MWA WENYE HALI MBAYA SANA.”

 

Basi hao wanawake wenye kuonesha miili yao ndio miongoni mwa hao inayowafuatia laana usiku na mchana, na siku ya Kiyama watakuwa wenye hali mbaya sana kwa kuasi amri yah ii, wakajishabihi kuwa sawa na makafiri. Wanaodhulumu nafsi zao kwa kufanya maasi haya ya kuonesha miili yao watu ajnabi, basi wao ni miongoni mwa watu madhalimu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Huud aya ya 18 amesema:-

 

“….. SIKILIZENI! (ENYI WATU!) LAANA YA MWENYEZI MUNGU IKO JUU YA MADHALIMU….”

 

Basi siku ya Kiyama hao madhalimu hawatakubaliwa kwao udhuru wowote ila wataangamia katika nyumba mbaya kabisa ya moto wa Jahannam.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Ghaafir (au Muumin) aya ya 52 amesema:-

 

“SIKU AMBAYO HAUTAWAFAA MADHALIMU UDHURU WAO NA WATAPATA LAANA, NA WATAPATA NYUMBA (YA MOTO WA JAHANNAM) ILIYO MBAYA KABISA.”

 

Na hao wanawake wenye kuvaa nguo za kikafiri na kuonesha miili yao kwa watu ajnabi wanadhulumu nafsi zao kwa kufanya maasi hayo. Basi wao ndio miongoni mwa hao madhalimu kwa kuasi amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kuasi amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo atapata adhabu ya nyumba mbaya katika moto wa Jahannam na akae humo milele. Wakati huo atakapoiona adhabu ya Jahannam atajuta kwa kuasi kwake, lakini hayo majuto hayatamfaa kitu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Jinn aya ya 23 amesema:-

 

“…… NA ANAYEMUASI MWENYEZI MUNGU NA MTUME WAKE, BASI (HUYO KAANGAMIA) ATAPATA (ADHABU YA) MOTO WA JAHANNAM AKAE HUMO MILELE.”

 

Na hao wanawake wasiostiri miili yao wanaowaigiza Mayahudi na Wakristo kuvaa nguo za kikafiri, basi hao si wanawake wa Kiislam bali wao ni makafiri kabisa. Wanaasi amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na gereza la makafiri ni Jahannam.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Israa aya ya 8 amesema:-

 

“….. NA TUTAIFANYA (ADHABU YA MOTO WA) JAHANNAM KUWA NI GEREZA LA MAKAFIRI.”

 

Na hao wanawake wenye kuvaa nguo za makafiri zisizokuwa za stara, wala hawaifuniki miili yao, wanaionesha ovyo tu, basi wanawake hao ni makafiri na gereza lao ni Jahannam linawangoja.

 

Enyi wanawake! Enyi akina dada na watoto wetu! Mcheni (muogopeni) Mwenyezi Mungu, liogopeni gereza la moto wa Jahannam, adhabu yake ni kali sana.

Huko kuvaa nguo za kubana na kuweka vichwa wazi na kupaka rangi za midomo na kufuga kucha ndefu na kuzitia rangi na kuvaa nguo fupi na kuonesha mapambo ya miili yenu. Yote hayo si maendeleo, bali huko ni kujiangamiza nafsi zenu.

 

Huko ni kuzifuata tabia mbaya za makafiri wa Kiyahudi na makafiri wa Kikristo na wapagani. Kufanya hivyo ni kujitoa, au mnajitoa wenyewe katika Uislam na kuingia katika ukafiri kwa khiari zenu. Hivi mmestahabu ukafiri kuliko Uislam, mmekiri kupata moto wa Jahannam kuliko kupata Pepo na radhi la Mola wenu.

 

Mnaziuza radhi za Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo ya upuuzi wa dunia na kununua hasira na ghadhabu za Mwenyezi Mungu.

 

Mwenyezi Mungu amekataza kuongea mwanamme na mwanamke ila mpaka iwepo kinga baina yao. Maana kuongea bila ya kinga basi watatu wao huwa Shetani, kama tulivyotaja katika hadithi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nyuma. Shetani huwatia maradhi nyoyoni mwao ya mambo mabaya ya uchafu wa zinaa na maradhi haya mara moja yanapatikana kwa watu.

 

Ndio Mwenyezi Mungu amewahutubia wake wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kawakataza wasiongee na wanaume ila iwepo kinga baina yao. Na hutuba ya Mwenyezi Mungu kwa wake wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi ndiyo hutuba ya waislam wote mpaka kisimame Kiyama.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al- Ahzab aya ya 32 amesema:-

 

“ENYI WAKE WA NABII (MUHAMMAD)! NYINYI SI KAMA YOYOTE KATIKA WANAWAKE (WENGINE), KAMA MNATAKA KUMCHA (MWENYEZI MUNGU) BASI MSILEGEZE SAUTI (ZENU MNAPOSEMA NA WANAUME) ILI ASITAMANI MTU MWENYE UGONJWA (WA MAMBO MACHAFU) MOYONI MWAKE, NA SEMENI MANENO YALIYO MEMA.”

 

 

 Na kama tulivyosema kuwa kukatazwa kwa wake wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio wanakatazwa wanawake wote wa Kiislam. Na baada ya kukatazwa wanawake wa Kiislam, basi pia amri hiyo wameamrishwa na wanaume vile vile, nao ni masahaba wake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al- Ahzab aya ya 53 amesema:-

 

“…… (ENYI WAISLAM!) NA MNAPOWAULIZA (WAKEZE MTUME) KITU, BASI WAULIZENI NYUMA YA KINGA. (KUFANYA) HAYO NI KUSAFISHA (FIKIRA MBAYA)  NYOYO ZENU (NYINYI WANAUME) NA NYOYO ZAO (WANAWAKE).”

 

Na kukatazwa hao masahaba basi ndio wanakatazwa wanaume wote wa Kiislam kuongea na wanawake bila ya hijabu (kinga).

 

Maana macho yanazini kwa kutazama, na ulimi unazini kwa maneno, na mkono unazini kwa kushika, na miguu inazini kwa kuliendea jambo chafu.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“IMEANDIKWA KWA BINAADAMU SEHEMU YAKE YA KUZINI ATAPATA TU (DHAMBI) HIZO HANA BUDI NAZO (IKIWA YEYE NI MWENYE TABIA HII CHAFU): MACHO KUZINI KWAKE NI KUTAZAMA, NA MASIKIO ZINAA KWAKE NI KUSIKILIZA (MANENO MACHAFU), NA ULIMI KUZINI KWAKE NI MANENO, NA MIKONO ZINAA YAKE NI KUSHIKA, NA MIGUU ZINAA YAKE NI HATUA (KULIENDEA JAMBO CHAFU), NA MOYO UNAANGUKA NA KUTAMANI, NA UNASADIKISHA HAYO UTUPU AU UNAMKADHIBISHA.”

 

Na katika hadithi ya bibi A’isha na Umm Salamah na Maimuna, wake wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  (Radhiya Allaahu ‘anhum). Amesema Umm Salamah kuwa:  Tulikuwa tumekaa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kutuamrisha kuhusu hijabu.

Basi mara akaingia Ibn Umm Maktuum, naye ni kipofu. Alipoingia tu pale tulipo, basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuamrisha tujifunike, akasema jifunikeni hijabu!…. Tukasema : Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Huyu ni kipofu hatuoni wala hatujui!… Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Jee! Kwani nyinyi ni vipofu vile vile? Nyinyi si mnamuona?…. Ina maanisha kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kawaamrisha wake zake wajifunike, ingawa yule ni kipofu haoni, lakini wao wanamuona.

 

Maana si hoja ya kuwa kipofu haoni basi wamkalie vichwa wazi, kwa kuwa yule hana macho ya kuona. Lakini masikio anayo anasikia, na mdomo anao anasema. Na kama tumekwishataja hadithi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa viungo hivyo pia vinazini.

 

Na mwanamke ameamrishwa akae nyumbani asitoke nje ila kwa dharura ya kutimiza hja zake zilizokuwa muhimu kwake. Na amri hiyo ya kukuamrishwa wanawake wakae majumbani mwao tumekwishaitaja katika Surat Al-Ahzab aya ya 33, anayosema:-

 

“NA KAENI MAJUMBANI MWENU……”

 

Na mwanamke khasa kaumbwa kwa ajili ya nyumba, kazi yake inayomkhusu khasa ni kazi za nyumbani, ama kazi za nje ni za wanaume. Pia mwanamke anaweza kutoka nje kama tulivyosema kuwa mwanamke atatoka nje kwa ajili ya kutimiza haja zake muhimu za sheria, na kutoka huko kuna masharti, na masharti yenyeqwe ni kwmaba austiri mwili wake, na wala asioneshe mapambo yake, na wala asipake mafuta mazuri.

 

Ana wanawake wengine hupenda kutoka makusudi ili aoneshe mapambo yake, khasa akiwa na nguo za kifahari na nzuri, ili aoneshe watu pambo la mwili wake. Na hii imethibitika katika sunna ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza wanaume kuwadekeza wake zao kwa kuwanunulia nguo kwa wingi na za ufahari, kwa sababu hiyo, maana akiwa na nguo nyingi na nzuri nzufri mwanamke hupenda avae mara kwa mara na kutoka nje mara kwa mara.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“JISAIDIENI JUU YA WANAWAKE KWA UWEKEVU (UZUIZI WA MAVAZI), BASI KWA HAKIKA MMOJA WAO WANAWAKE ZIKIZIDI KUWA NYINGI NGUO ZAKE NA MAPAMBO YAKE YAKIWA MAZURI (BASI) HUPENDA ATOKE.”

 

Hapa ina maanisha kuwa mwanamke akiwa na nguo nyingi sana na mapambo mazuri mengi, basi anataka atoke nje mara kwa mara ili awaoneshe watu huko nje uzuri wa mapambo yake, na huzidi kiburi chake. Na ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anawaambia wanaume wasiwalegezee wanawake kwa kuwanunulia nguo kwa wingi, na wazuie.

Na akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):-

 

“ZUIENI (KWA MAVAZI MENGI YA) WANAWAKE (MKIFANYA HIVYO) WATAJISTIRI (MIILI YAO).”

 

Na mradi si kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewakataza wanaume wasinunue nguo wake zao, bali anawahimiza wanaume kuwavisha wake zao, na khasa ni kwamba wasiwadekeze kwa kuwanunulia nguo nyingi sana zilizokuwa za fakhari, hayo ya ufakhari ndio yanayomfanya mwanamke azuzuke kwa kutoka nje sana, na kuonesha mapambo ya mwili wake kwa wanaume ajnabi. Hayo mapambo yake na amvalie mumewe nyumbani, au wale waliotajwa katika Surat An- Nuur aya ya 31 kama tuliyokwisha ifasiri hapo nyuma.

 

Na pia wanawake wamekatazwa kutoka nje na hali ya kuwa wamejipaka mafuta mazuri, ampakie mumewe nyumbani tu, lakini akitoka nje ajioshe hayo manukato. Na mwanamke hata ikiwa amejifunika mwili wake gubi gubi lakini ananuka mafuta mazuri na katika nje, basi mwanamme, yeyote atakaeisikia harufu ya manukato ya huyo mwanamke, basi huyo mwanamke kazini, na anapata dhambi za kuzini.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“MWANAMKE YEYOTE YULE KAJIPAKA MAFUTA MAZURI AKAPITA KARIBU NA WATU WAKAPATA (WALE WATU) KUNUSA HARUFU YAKEBASI YEYE MWANAMKE KAZINI.”

 

Vile vile Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“MWANAMKE AKIJIPAKA MAFUTA MAZURI BASI AKAPITA MAJLIS, BASI YEYE KAZINI.”

 

Wataalamu wameifasiri hadithi hii kuwa mwanamke ikiwa kajipaka mafuta mazuri kasha akapita majlis ile harufu humo majlis na mara tu wakaingia wanaume humo majlis wakaisikia harufu ile ya manukato iliyotoka kutoka kwa yule mwanamke, basi yule mwanamke kazini.

 

Ingawa wale watu hawakumuona yule mwanamke, lakini sababu ile harufu imetokana na yule mwanamke aliyepita pale majlis ikabaki ile harufu humo majlis.

 

Na kama tulivyosema kuwa hata ajisitiri vipi mwanamke, lakini ikiwa katoka nje naye inamtoka harufu ya manukato ya mafuta mazuri, basi yeye anapata dhambi za kuzini, na mwili wake unakuwa katika hukumu ya mwenye janaba, haikubaliwi ibada yake yoyote ila mpaka akaoge uogaji wa janaba.

 

Baada ya kufa Nabii Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), siku moja ilikuwa siku ya Ijumaa, Sahaba Abu Hurairah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa anakwenda Msikitini katika sala ya Ijumaa, alipofia karibu na Msikiti akakutana na mwanamke mmoja hapo karibu na Msikiti. Yule mwanamke alikuwa kajistiri mwili wake vizuri, kajifunika gubi gubi, na ananuka manukato ya mafuta mazuri.

 

Abu Hurairah (Radhiya Allaahu ‘anhu)  ikamjia ile harurfu ya manukato kutoka kwa yule mwanamke, na yule mwanamke alikuwa amekaza mwendo kuikimbilia sala ya jamaa hapo msikitini. Basi Abu Hurairah (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwambia yule mwanamke: Ewe mwanamke mbona umekaza mwendo unaelekea msikitini?… Akasema yule mwanamke kwamba nakimbilia sala ya jamaa!…      Akasema Abu Hurairah ya kwamba: Vipi unaikimbilia sala ya jamaa na hali wewe umezini? Nenda kwanza kaoge, kasha ndio uje kusali, jee! Hujui kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema ya kwamba mwanamke akijipaka mafuta mazuri manukato yake akibusa mtu basi yeye kazini?.. Na wewe unanuka mafuta mazuri, nimenusa manukato kutokana na wewe, jee! Hujui kuwa umezini?.. Wewe sasa umo katika hukumu ya mwili mchafu wa janaba, basi nenda kwanza kaoge kasha ndio uje kusali.

 

Abu Hurairah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kamhukumu yule mwanamke kuoga, na hakumruhusu kusali. Sasa hayo ni mafuta mazuri tu mwanamke anapata madhambi ya kuzini.

Na akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):-

 

“ANAPOHUDHURIA MSIKITINI MMOJA WENU (NYINYI) WANAWAKE BASI MSIYAGUSE MAFUTA MAZURI.”

 

Na akazidi kusema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):-

 

“BORA YA MAFUTA MAZURI YA WANAUME NI YENYE KUTOA HARUFU YAKE NA HAIONEKANI (IMEFIFIA) RANGI YAKE. NA BORA YA MAFUTA MAZURI YA WANAWAKE NI YENYE KUONESHA (KUKOZA) RANGI YAKE NA KUFIFIA (YASIYOTOA) HARUFU YAKE.”

    

Na akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):-

 

“MWANAMKE YEYOTE YULE KAJIPAKA MAFUTA MAZURI KWA AJILI YA (KWENDA) MSIKITINI (BASI) HAIKUBALI MWENYEZI MUNGU SALA YAKE MPAKA (KWANZA) AOGE UOGAJI WA JANABA.”

 

Sasa hayo ni mafuta mazuri tu hatari hiyo anaipata mwananmke kwa kupata dhambi za kuzini na kuwa mwili wake katika hukumu ya mwenye janaba. Seuze mwanamke alieacha kichwa chake wazi, au kuvaa nguo za kubana, nguo ambazo si za stara, mwili wake wote unaonekana na watu, jee! Huyo kuhumu yake ni ya hatari zaidi kuliko hayo manukato au mafuta mazuri?  Huyo ndiye mwenye dhambi kubwa kabisa ya kuzini za daraja ya juu kabisa, laana ya Mwenyezi Mungu iko juu yake usiku na mchana.

 

Na hayo ndiyo yanayopita na kufanywa na wanawake wa Kiislam siku hizi; kuacha vichwa wazi, au atafunika kichwa lakini hiyo nguo aliyoivaa ni nguo ya kikafiri ya kubana, na wala kahuvaa baibui, mwili wake wote unaonekana, na uso umepiga weupe wa kishetani kwa mapodari na rangi za midomo, na rangi za mikiyaji machoni na mashavuni, na rangi za kucha, na viatu vyenye visigino vya ncha kumi, na kila aina ya mapambo ya mwili wake yanaonekana.

 

Yeye na shetani wa Kiyahudi ay Mkristo hakuna tofauti yoyote. Sasa huyo tutamwita kuwa yeye ni mwanamke wa Kiislam? Huyo ni mwanamke kafiri mkubwa, laana za Mwenyezi Mungu  ziko juu yake. Anaacha adabu na tabia za Kiislam, ameshika na kufuata tabia za makafiri wa Kiyahudi, Kikristo na wapagani.

 

Amesema bibi A’isha (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa; “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kawalaani wanawake wenye kukwaruza (kunyofoa) nyusi zao usoni na kuchonga meno, na kubandika nywele za mapambo vichwani, wanabadili umbo la Mwenyezi Mungu.”

 

Na haya ndiyo yanayofanywa na wanawake wa Kiislam siku hizi. Wanajipamba mapambo yaliyopindukia mipaka na sheria za Kiislam mpaka wanajibadilisha umbo alilowaumbia Mwenyezi Mungu. Na hayo mapambo ndiyo yanawasababishia watoke nje ili waoneshe hayo mapambo yao na kuonesha miili yao wanaume ajnabi huko nje. Na hali mwanamke ameamrishwa asitoke nje ila kwa jambo la dharura.

 

Na akitoka nje kwa sababu ya kisheria, basi pia pana masharti ya kutoka kwake, austiri mwili wake kwa vazi la Kiislam, wala asipake mafuta mazuri na asijifukize udi, na anapopita njiani ainamishe macho yake pamoja na kutotizama machafu yaliyokatazwa, na mengineyo yaliyoamrishwa katika Uislam. Kutoka kwake kuwe kwa heshima na adabu, na kuwa na hadhari sana asisababishe fitina (mitihani) kwa wanaume huko nje. Maana mwanamke ni fitna kubwa kwa wanaume.

 

Mwanamke akitoka nje lazima achukue hadhari kubwa sana, hata ikiwa anakwenda Msikitini na asitoke ila kwa baada ya kupata ruhusa kwa walii wake au mumewe.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“AKIKUOMBENI IDHINI MMOJA WENI MKEWE KWENDA MSIKITINI BASI ASIMKATAZE.”

 

Kwa mujibu wa wataalamu walioifasiri hadithi hii wameifasiri kwamba, huyo mwanamke atekeleze hayo masharti tuliyoyataja ya kujistiri mwili wake, na kutoyagusa kabisa manukato au mafuta mazuri. Na pia kuruhusiwa huko kwenda Msikitini kwa ajili ikiwa huko Msikitini kuna mawaidha ya dini ambayo hayapati nyumbani kwake ila mpaka aende Msikitini, kwa masharti hayo ndiyo ameruhusiwa kwenda Msikitini.

 

Ama ikiwa anatoka kwenda Msikitini kwa ajili ya sala basi ni bora kwake asali nyumbani kwake au kwao kuliko kuifuata sala ya jamaa Msikitini, maana sala ya mwanamke ya Msikitini masharti yake ni makubwa sana, na thawabu zake ni ndogo sana, ila akitimiza hayo masharti kwa kuyatekeleza ndio huenda akapata daraja ya thawabu ya sala ya jamaa.

 

Ina maanisha kuwa kutoka kwake mwanamke kwenda Msikitini basi ni mtihani mkubwa kwa wanaume kuho nje, humo njiani wamejaa mashetani, ikiwa sababu ya kufitinika wanaume, na ikawa kazi ya bure, badala ya hayo mwanamke kupata thawabu ya sala ya jamaa, akazikosa hizo fadhila za sala, na matokeo yake ikawa kaenda kappa (bila ya kupata chochote) na kupata madhambi. Ndio Mtume akawahimiza wanawake sala za majumbani mwao ni bora kuliko sala za jamaa Misikitini.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“SALA ZAO WANAWAKE KATIKA MAJUMBA YAO NI BORA KWAO, NA WAKITOKA (KWENDA MSIKITINI) BASI WATOKE WAMEJISIRI (SANA MIILI YAO) KWA NGUO ZA STARA, WALA WASIYAGUSE MAFUTA MAZURI).”

 

Sasa hadithi hii mwanzo wake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anakataza wanawake kuziendea sala za jamaa huko Misikitini anawatakia kheri ili waepukane na hizo fitna (mitihani) ya Kishetani, na ili sala zao zisipotee ikawa kazi ya bure. Na mwisho wa hadithi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametoa masharti, ikiwa watatoka kwenda huko Msikitini basi watekeleze hayo masharti ya kutoka kwa adabu, na waistiri miili yao, na wala wasiyaguse mafuta mazuri au manukato.

Na akazidi kusema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):-

 

“BORA YA MISIKITI YA WANAWAKE NI NDANI YA NYUMBA ZAO.”

 

Pia kasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):-

 

“…. SALA YA MWANAMKE KATIKA NYUMBA NI BORA KULIKO KUSALI KATIKA MSIKITI.”

 

Na imethibiti katika sunna ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kwamba mwanamke sala yake moja nyumbani kwake anapata daraja ishirini na tano. Kwa hiyo sala ya mwanamke nyumbani kwake ni bora kuliko sala ya jamaa Msikitini.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“(MWILI WA) MWANAMKE NI UCHI, AKITOKA (NJE, BASI) SHETANI HUMKALIA MBELE YAKE, NA ANAKUWA KARIBU SANA NA (RADHI ZA) MWENYEZI MUNGU KILA ANAPOKUWA NYUMBANI KWAKE.”

 

Hapa ina maana kuwa mwanamke akitoka nje kama hakuchukua hadhari ya kutekeleza sheria za uislam, basi huyo hana salama, au hatasalimika na kuopta madhambi ikiwa hakuchukua hadhari. Na kila akiwa nyumbani kwake, basi hupata radhi na maghfira (msamaha) kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na mwanamke kukaa nyumbani kwake, basi anapata fadhila kubwa sana kwa Mola wake.

 

Ama wanawake wenye kupenda kutoka nje mara kwa mara, na kuonesha mapambo yao, na kuonesha miili yao ovyo huko nje bila ya khofu yoyote, basi hao si wanawake wa Kiislam, hao nimakafiri tu, laana na ghadhabu za Mwenyezi Mungu iko juu yao. Ibada yao haipandishwi juu mbinguni hata shibiri moja.

 

Enyi wanawake wa Kiislam iogopeni hasira ya Mwenyezi Mungu, adhabu zake ni kali sana. Jueni kwamba Uislam ni neema kubwa sana, na fadhila zake ni kubwa sana. Nanyi mnazikataa neema za uislam na fadhila zake, kasha wenyewe mnaingia katika ukafiri, kwa kutokutekeleza amri zilizoletwa katika Uislam, pana tofauti gani baina ya hao wanawake wenye kuonesha miili yao wanaume ajnabi na makafiri?  Hakuna tofauti yoyote na makafiri.

 

Na wale wanawake wa Kiislam wenye kustiri miili yao na kuvaa nguo za Kiislam, na kutekeleza amri hii, basi wanachekwa na kupuuzwa na kuwekwa nyuma kabisa kwa ajili ya kutekeleza amri hii. Basi kama wanvyochekwa hapa duniani, basi na wao watawacheka hao wenye kuwacheka siku ya Kiyama. Na watapata thawabu zao nzuri nzuri kwa subira waliyoichukua hapa duniani kwa kutii amri ya Mola wao ya kusitiri miili yao na kutekeleza amri nyengine za Uislam.

 

Na hao wenye kuipuuza amri hii wataona siku ya Kiyama yatawafika, majuto yao hayatawafaa kitu, bali hayo majuto yao yatawaangamiza katika nyumba ya moto wa Jahannam kwa kuwapuuza na kuwacheka wanawake wenzao wenye kusitiri miili yao.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Mutaffifiina aya ya 29 amesema:-

 

“KWA HAKIKA WALE WALIOKUWA WAKIFANYA MADHAMBI (MAASI) WALIKUWA WAKIWACHEKA WAISLAM – NA WANA[POPITA KARIBU YAO WAKIKONYEZANA – (KWA KUWAPUUZA WAISLAM WALIOTII AMRI ZA MOLA WAO) NA KUWACHEKA – NA (HAO WENYE KUASI AMRI ZA MOLA WAO) WANAPOWAONA (WAISLAM WALIOTII AMRI ZA MOLA WAO, BASI) HUSEMA (HAO WAOVU): HAKIKA HAWA (WAISLAM WENYE KUTII AMRI ZA MOLA WAO) NDIO (WAJINGA NA) WALIOPOTEA (NA WATU WA NYUMA KABISA) -… BASI LEO (SIKU YA KIYAMA) WAISLAM WATAWACHEKA WALIOKUFURU (KAMA WALIVYOKUWA WAKICHEKWA DUNIANI), (HAO WAISLAM WATAKUWA WAMEKAA) JUU YA VITI VYA FAGHARI WAKITAZAMA (NEEMA ZA PEPONI WALIZOPEWA, HUKU WAKIWACHEKA HAO MAKAFIRI).”

 

Na katika Surat Muuminuun aya ya 110/111 Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:-

 

“BASI NYINYI MLIWAFANYIA MASKHARA (WAJA WANGU WALIOTII AMRI ZANGU) HATA WAKAKUSAHAULISHENI KUNIKUMBUKA, NA MLIKUWA MKIWACHEKA – (BASI) HAKIKA MIMI LEO (SIKU YA KIYAMA) NIMEWALIPA (PEPO) KWA SABABU YA KUSUBIRI KWAO (KWA AJILI YA KUTII AMRI ZANZGU) HAKIKA WAO NDIO WALIOFUZU.”

 

Basi nyinyi wanawake wa Kiislam wenye kutii amri za Mola wenu, mkastiri miili yenu kwa mavazi ya Kiislam, subirini na vumilieni katika kutekeleza amri ya Mola wenu, wala wasikushitueni hao wanaokuchekeni kwa kutekeleza amri hii ya Mwenyezi Mungu, malipo yenu yatakuwa mazuri kabisa. Na dunia ni jela ya Waislam, na Pepo ya makafiri na wavunjao amri.

 

Na akhera ni Pepo ya waislam na jela ya makafiri. Na Muislam mwenye kutekeleza amri za Mola wake, basi akifa tu anafurahi sana, maana anatoka gerezani (jela) na kuingia Peponi. Papo hapo anapotolewa roho Muislam, basi Malaika wanampa pongezi ya kutoka  jela na kupata Pepo achukue uhuru wake kamili huko Peponi, afanye analopenda, na atapata kila anachokitamani.

 

Lakini kafiri akifa tu, basi papo hapo Malaika wanambashiri kwa kutoka katika Pepo ya dunia na kuingia katika gereza (jela) la moto wa Jahannam.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Israa aya ya 8 amesema:-

 

“…. NA TUKAIFANYA (ADHABU YA MOTO WA) JAHANNAM KUWA NI GEREZA LA MAKAFIRI…..”

 

Basi enyi wanawake, wenye kupuuza amri hii ya kustiri miili yenu, tunakuoneni na kukuhadharisheni, na kukufikishieni mawaidha ya Mwenyezi Mungu, mcheni (muogopeni) Mola wenu na mtubie kwa majuto, na wacheni kuvaa nguo za kikafiri, na vaeni nguo za Kiislam ndio mtasalimika.

 

Na mwenye kupuuza mawaidha haya ya Mwenyezi Mungu, basi maisha ya dhiki ya adhabu za kaburini na Akhera zinawangojea.

 

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al- Ahzab aya ya 32 amesema:-

 

“NA MWENYE KUPUUZA MAWAIDHA YANGU (HAYA), BASI KWA HAKIKA ATAPATA MAISHA YENYE DHIKI, NA SIKU YA KIYAMA TUTAMFUFUA NA HALI YA KUWA (YEYE NI) KIPOFU.”

 

Na maisha ya dhiki yaliyotanjwa katika aya hii kaifasiri Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba ni maisha ya adhabu ya kaburini. Basi mcheni (muogopeni) Mola wenu kwa kutekeleza amri zake zote, na mtubie toba ya majuto, na mtengeneze mliyoyabomoa kabla ya kukupiteni wakati mkafa bila ya kuzinduka.

 

Maadamu roho bado zingali hai mwilini basi zindukeni mjitayaraishe kuchukua masururfu yatakayoweza kukusaidieni huko mnakokwenda makaburini na Akhera. Maana inahitaji masurufu (matumizi) ya kutumia katika safari, msiende mikono mitupu mkamtegemea Shetani, bali Shetani kazi yake kudanganya na kuangamiza tu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Baqarah aya ya 208 amesema:-

 

“ENYI WAISLAM! INGIENI KATIKA HUKUMU ZOTE ZA KIISLAM, WALA MSIFUATE NYAYO ZA SHETANI, KWA HAKIKA YEYE (SHETANI) NI ADUI KWENU ALIYE DHAHIRI.”

 

Chama cha Shetani ni cha kuangamiza tu katika adhabu kali ya Mwenyezi Mungu. Basi jiepusheni na huyo adui yenu mkubwa, na mtubie toba ya kweli, na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu kwa mwenye kutubia kasha akatekeleza amri zake zote. Na Mwenyezi Mungu pia ni mkali wa kuadhibu kwa wasiotubu na wakaendelea kufanya maasi.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Hijr aya ya 49/50 amesema:-

 

“(EWE NABII MUHAMMAD!) WAZINDUE WAJA WANGU (UWAAMBIE) YA KWAMBA MIMI NI MWINGI WA KUSAMEHE (NA) MWINGI WA KUREHEMU – NA HAKIKA ADHABU YANGU BI ADHABU IUMIZAYO SANA.”

 

Basi enyi wanawake yazingatieni hayo mawaidha ya Mola wenu, na sitirini miili yenu ili msalimike na hizo adhabu za Mwenyezi Mungu zilizo kali sana. …. Kwanza ikiwa mwanamke kava nguo za Kiislam, na kafunika mwili wake vizuri, naye anapita njiani, basi mwanamme akimuona tu huyo mwanamke, basi atamuogopa, akiwa huyo mwanamme ana tabia mbaya basi hatathubutu kumuudhi, atajua kuwa huyu ni mwanamke mwenye heshima, atamheshimu na kumuogopa.

 

Ama ikiwa mwanamke anapita njiani hakujistiri mwili wake, viungo vyote vya mwili wake vinaonekana, basi hatasalimika kwa udhia. Maana akipita mbele za wanaume wenye tabia mbaya, basi lazima watamkonyeza, au kumfanyia jambo lolote baya, hatasalimika na udhia wowote humo njiani, na juu ya hayo anachuma madhambi.

 

Tunayaona haya mara nyingi sana wanafikwa wanawake wasiojistiri miili yao mabarabarani, ama watakonyezwa au watakamatwa, au kutupiwa maneno ya utovu wa adabu kutoka kwa wanaume wenye tabia mbaya, na sababu ya kufikwa na hayo ni mwanamke mwenyewe kutoka nje bila ya sharia za Uislam.

 

Na mwanamke ikiwa anatoka nje kwa safari zake, basi asipite kati kati ya njia, bali apite pembeni  mwa njia na awe mbali na watu, na awe kainamisha macho yake, na awe mwenye kujiheshimu ili aheshimiwe na aepukane na udhia wa humo njiani.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“HAIWI KWA MWANAMKE (KUPITA) KATIKATI YA NJIA.”

 

Basi mwanamke akitekeleza hukumu zote za Uislam na kuwa na adabu za Kiislam hafikwi na udhia wowote humo njiani, bali husalimika na kila jambo baya, na kila atakayemuona humo njiani basi atamheshimu, kwa kuwa kajistiri mwili wake, na anapita kwa adabu za kumcha (kumuogopa) Mola wake. Na fadhila zake ni kubwa sana.

 

 

 

BAADHI YA FADHILA KWA WANAWAKE NA BAADHI YA HUKUMU ZAO NA MENGINEYO KWA UFUPI

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“MWANAMKE YEYOTE YULE AKIINGIA MSALANI (CHOONI) BILA YA SABABU (MUHIMU) WALA UGONJWA (LAKINI KWA AJILI YA) KUJITAZAMA WEUPE (WA PAMBO) LA USO WAKE, BASI MWENYEZI MUNGU ATAUFANYA USO WAKE KUWA MWEUSI SIKU (YA KIYAMA, AMBAYO SIKU HIYO NYUSO ZA WAISLAM) ZITAKAPOFANYWA KUWA NYEUPE.”

 

Na maana ya hadithi hii ni kwamba, baadhi ya wanawake wakienda kutembea katika nyumba za watu, basi ataingia chooni (msalani) bila ya sababu yoyote iliyo muhimu, lakini kwa ajili ya ya kujitazama pambo la uso wake, kama podari na rangi za midomo na mikiyaani mapambo mengine ya uso, ili aoneshe vizuri hayo mapambo ya uso wake kwa watu.

 

Ndio wanawake wa siku hizi utaona handbag haimtoki mkononi, akitoka basin a handbag yake kaichukua, humo ndani ya handbag hiyo vimejaa vitu vya mapambo na kioo kidogo. Basi kila mara anatoa kioo kujitazama pambo la uso wake, ikiwa kitu kidogo tu usoni mwake kimeharibika, kama podari au rangi, basi atajitengeneza uso wake upya.

 

Basi wanawake wenye tabia hiyo kutia mapodari na rangi za nyuso kutaka weupe wa uso na rangi za midomo, basi siku ya Kiyama nyuso zao zitakuwa nyeusi na kuangamia katika Jahannam.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Aal – Imraan aya ya 106/107 amesema:-

 

“SIKU (YA KIYAMA) AMBAYO NYUSO (NYENGINE) ZITAKUWA NYEUSI, (BASI WATAAMBIWA:) JEE! MLIKUFURU BAADA YA IMANI YENU? BASI ONJENI ADHABU (KALI SANA) KWA KULE KUKANUSHA KWENU. AMA WALE AMBAO NYUSO ZAO ZITAKUWA NYEUPE, BASI WATAKUWA KATIKA REHEMA YA MWENYEZI MUNGU, WAO HUMO WATAKAA MILELE.”

 

Basi hao wanawake wenye tabia ya kupaka mapodari na rangi za midomo na mengineyo yanayobadili umbo la Mwenyezi Mungu, ndio watakuwa miongoni mwa hao watakaofanywa kuwa nyuso zao nyeusi siku ya Kiyama, ikiwa hawatotubu na wala hawatokoma kuwaigiza makafiri.

 

Na mwanamke baada ya kutekeleza amri za Mola wake, basi pia atekeleze amri za mumewe, amtii katika mambo yanayomridhisha mumeweambayo yameamrishwa na Mweyezi Mungu na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akifanya hivyo basi kafuzu kwa kupata radhi na Pepo ya Mwenyezi Mungu.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“AKISALI MWANAMKE SALA ZAKE (ZA FARADHI)TANO, NA AKAFUNGA MWEZI WAKE (WA RAMADHANI), NA AKAMTII MUMEWE, NA AKAHIFADHI UTUPU WAKE (KWA KUTOZINI NJE), (BASI HUYO) ANAINGIA PEPONI.”

 

Kasha atekeleze amri zote zilizoletwa katika Uislam, basi huyo amestahiki kupata radhi za Mwenyezi Mungu na Pepo yake. Lakini akienda kinyume na hayo basi kaangamia.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“AKIMWITA MMOJA WENU MKEWE KITANDANI KWAKE (KUMUINGILIA), BASI AKIKATAA MKE KWENDA (KUTIMIZA HAJA YA MUMEWE), (BASI YULE MKE) ANALAANIWA NA MALAIKA MPAKA ASUBUHI.”

 

Na katika hadithi nyengine Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa analaaniwa yule mwanamke mpaka mumewe awe radhi. Na katika hadithi nyengine ya kwamba, sala ya huyo mwanamke au ibadayake yoyote haipandishwi mbinguni hata shibiri moja. Tazama katika kitabu cha “ Mkweli Muaminifu” Juzuu ya pili, ambapo yametajwa mambo haya kutoka katika hadithi nyingi sana za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mke amtii mumewe na kumridhisha hata katika mambo haya. Lakini asimtii kwa kuingiliana nae akiwa katika hali ya hedhi, au kwa utupu wa nyuma, ambayo ni mambo ya maasi anatakiwa asimtii. Haijuzu kumtii kiumbe katika kumuasi Mwenyezi Mungu.

 

Vile vile haijuzu kwa mwanamke kumuongopea (kumdanganya) mumewe, wakati mumewe anapotaka kutimiza haja yake mwanamke akajizungusha au aseme kuwa ana hedhi. Mwanamke wa aina hiyo analaaniwa na Mwenyezi Mungu.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“AMELAANIWA NA MWENYEZI MUNGU MWANAMKE MWENYE ILA (INDA), AMBAYE AKITAKA MUMEWE KUMUINGILIA ANASEMA MIMI NINA HEDHI.”

 

 

FADHILA ZA KUBEBA MIMBA NA UZAZI

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:-

 

“HAKIKA (FADHILA) ANAZOZIPATA MWANAMKE KATIKA KUBEBA KWAKE MIMBA MPAKA KUZAA MPAKA (KUNYONYESHA, NA MPAKA) KUMUACHISHA ZIWA (MTOTO) MALIPO (YA THAWABU ZAKE) KAMA ALIYEKUWA JIHADI ANAWATUMIKIA (WANAOPIGANA JIHADI) KATIKA NJIA YA MWENYEZI MUNGU. NA AKIFA KATIKA BAINA (YA MUDA) HUO BASI ANAPATA UJIRA WA SHAHIDI.”

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kawauliza masahaba wake: Jee! Nani na nani mnahisabu kuwa wao ni mashahidi?  Wakamjibu ya kwamba: Mwenye kupigana jihadi akauawa! … Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kwamba basi (mashahidi) ni kidogo sana ikiwa wanaouwawa jihadi tu. Kasha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuwaambia ya kwamba:-

 

“MASHAHIDI WA UMMA WANGU NI: ANAYEUAWA KATIKA NJIA YA MWENYEZI MUNGU (YEYE) NI SDHAHIDI, NA ANAEZAMA (BAHARINI AU KATIKA MAFURIKO YA MAJI) NI SHAHIDI, NA (ANAEKUFA KWA UGONJWA WA) TAUNI SHAHIDI, NA MWANAMKE ANAEKUFA KWA AJILI YA UZAZI NI SHAHIDI.”

 

Na mashahidi wa aina nyingi kawataja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), miongoni mwao ni wanawake wenye kufa kwa ajili ya mamba au kujifungua (kuzaa) au katika jambo lolote linalohusu uzazi, basi wao wanapata thawabu za daraja za mashahidi.

 

Walikuja wanawake kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wanaume wanakwenda jihadi, na wanapata fadhila za jihadi, jee! Sisi wanawake hatuna kazi ya kufanya hata tupate na sisi fadhila za jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu! …..   Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):-

 

“KAZI YA MMOJA WENU KATIKA NYUMBA YAKE BASI ANAFIKIA (FADHILA) ZA WANAOFANYA JIHADI KATIKA NJIA YA MWENYEZI MUNGU.”

 

Na furaha ya maisha ya mtu, basi awe na mke mwema, anaetekeleza amri za Mwenyezi Mungu, na kumtii mumewe. Huyo ndiye mwanamke mwema, na ndiye atakaefanikiwa (atakaefuzu) duniani na Akhera.

 

Basi enyi wanawake mcheni (muogopeni) Mwenyezi Mungu na mtekeleza amri zake na za Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili mfanikiwe (mfuzu) duniani na Akhera.

 

Tunamuomba Mwenyezi Mungu awaongoe wanawake wote wa Kiislam wakubwa na wadogo na waso waislam waione haki na wawe na upeo wa kutambua haki na batili. Waongoke katika kuepukana na tabia za kikafiri, na watekeleze katika kufanya yanayoamridhisha Mwenyezi Mungu. Namuomba mola wangu awanufaishe wasomaji wa Makala hii, na aiweke kazi hii mbali na sifa au mambo ya Kiulimwengu, bali aifanye kwa ajili ya kutaka radhi na maghfira na rehma zake, na malipo yake yawe Pepo.

 

AAMIN

 

WASSALAM ALEYKUM WARAHMATULLAHI WABARAKATUH. WASSALATU WA SSALAM ALAA RASUULIHI KHAATAMI NNABIYYIYA MUHAMMAD , WA ALAA AALIHI WASAHBIHI AJMIYN

 

 

 NAFASI YA MWANAMKE KATIKA TAMADUNI TAFAUTI

 UTANGULIZI:

Kuna hatua mbili muhimu za kuelewa nafasi ya mwanamke katika Uislamu. Hatua ya kwanza ni kuangalia nafasi ya mwanamke katika tamaduni zisizo za  kiislamu. Hatua ya pili ni kufanya somo linganishi baina yao. Tutapofanya hivyo tutagunduwa kuwa:

Uislamu umeipa familia nafasi na umuhimu wa pekee. Mfumo wa kifamilia katika Uislamu unatowa haki kwa mume, mke, watoto, ndugu na jamaa kwa uwiano ulio wazi. Ni mfumo unaopinga tabia za uchoyo, umimi na wivu. Mapenzi ndiyo kiini cha mjengeko wa familia katika mafunzo ya Kiislamu.

Nafasi na haki za mwanamke katika jamii akiwa ameolewa au hana mume imewekwa wazi ikiwa ni pamoja na kumiliki na kutumia mali yake bila ya kuingiliwa au kusimamiwa na yoyote. Bali kwa lengo la kuondosha dhulma, udhalilishaji, unyanyasaji na ukandamizaji kwa mwanamke unaofanywa na tamaduni zisizo za Kiislamu, au waislamu wasiofuata mafunzo ya Uislamu ndiyo mana Mtume SAW akawasisitizia waislamu ubora wa kufanya usawa na uadilifu kwa wanajamii wote kwa kusema katika Hadithi kuwa: ((waliobora miongoni mwenu ni wale walio wema kwa wake zao)) Ibn Majah na Tirmidhi.

MWANAMKE KATIKA TAMADUNI NYENGINE:

Katika Encyclopedia Britannica, 11th ed., vol. 28 pamesemwa: “Katika India, mwanamke kuwa mtegemezi ni jambo la msingi kabisa. Ni lazima mwanamke awe chini ya kinga ya mwanamume. Haki ya kurithi ni ya mwanamume pekee ambaye anahaki ya kumrithi hata mwanamke”  Aidha, katika maandiko ya Kihindu, pametajwa kuwa sifa za mke mzuri ni pamoja na hizi zifuatazo: “….akili yake, mwili wake na maneno yake ameyaweka chini ya utegemezi wa mumewe” sifa hizi zimetajwa na Vera katika “Marriage East and West”

Katika Athens, E.A Allen “History of Civilization” pameelezwa kuwa: “Mara zote wanawake wa Athena walikuwa ni wategemezi kwa baba zao, ndugu zao wa kiume au wanaume wengine,… haki yake ya kuolewa haikutiwa maanani, alitakiwa afuate tu matakwa ya wazee wake ikiwa ni pamoja na kupokea mume hata kama hakumjuwa au hakumpenda.

Katika Encyclopedia Britannica pameelezwa tena kwamba “Katika sheria za Roma, mwanamke alikuwa kwa ujumla wake ni tegemezi. Anapoolewa, yeye na mali zake zote zinakuwa za mumewe, ….mwanamke alikuwa ni bidhaa kwa mumewe. Mwanamke hakuwa na haki yoyote ya kiraia”.

Mwanahistoria mkubwa wa Kigiriki, Herodolt ametowa taarifa isemayo kwamba Ashtar alikuwa ni Mungu wa Waforsi wa mapenzi na uzuri. Moja kati ya matambiko kwa dini yao ilikuwa ni kutowa muhanga mwanamke mzuri aliye bikra. Mwanamume yeyote anayetaka kuoa ilikuwa anatakiwa kupeleka kipande cha shaba katika hekalu la mungu huyu na kumchukuwa  mwanamke huyo kwenda naye atakako.

Katika ustaarabu wa Kaldonia, mwanamke aliyekuwa hajapata ujauzito muda mfupi baada ya ndoa yake huonekana kuwa amelaaniwa na miungu, Hupelekwa kufanyiwa dawa na asipopata uja uzito anaweza kuuliwa ili roho yake ikastarehe pahala pema.

Katika Misri ya kale, mwanamke alikuwa na aina fulani ya uhuru wa kurithi na kumiliki nyumba wakati mumewe anapokuwa hayupo. Hata hivyo alikuwa hana thamani kubwa kwa vile baadhi ya wanawake walikuwa wakitolewa muhanga kwa miungu na kwa kutupwa katika mto Nile ili uendelee kutowa neema kwa watu wa Misri.

Katika Uyahudi, mwanamke yoyote asiye Muyahudi alionekana ni sawa na mnyama. Kwa hivyo kumuadhibu haikuwa kosa. Mwanamke hakuwa na uhuru wa kukataa tendo lolote analolitaka mume katika nyumba yao. Baba alikuwa na haki ya kumuuza mtoto wake wa kike.

Baadhi ya dini za Ulaya zinaamini kwamba mwanamke ndiye chanzo cha shari na matatizo yote yanayomkumba binaadamu. Hii ni kwa sababu Bi Hawa ndiye aliyekosea kwa kumlaghai Adam hata wakatolewa peponi.

Katika Ulaya kulifanyika mkutano wa kidini huko Ufaransa katika mwaka 586 CE na pakakubaliwa kwamba ukimtowa bikira Maria, wanawake wote si wakamilifu. Miongoni mwa masuali yaliyoulizwa katika mkutano huo ni pamoja na: Je mwanamke ni roho tupu au ana roho na kiwiliwili? Je mwanamke ni binaadamu au hapana? (M. Cisse, 2005, 4). Mwanamke wa Uingereza amepewa uhuru wa kumiliki mali yake mwenyewe Mnamo mwaka 1882 (ibid, 4), Mwanamke wa Ufaransa amepewa uhuru kamili mnamo karne ya 18.

Katika Waarabu wa zamani/Jahilia, mwanamke alikuwa ni alama ya unyonge. Hawakusherehekea anapozaliwa mtoto wa kike. Palikuwa na uhuru wa kumdhalilisha hadi kumuuwa wakati mwengine. Aidha mwanamke anayeachwa hai alikuwa ni sehemu ya rasilimali ya mwanamume, kwa hivyo wajane walikuwa wakirithiwa.

Mwanamume alikuwa na haki ya kuoa idadi yoyote ya wake bila ya kushauri na akitaliki atakavyo bila ya kizuwizi

MWANAMKE KATIKA UISLAMU 

Miongoni mwa lengo la Uislamu ni kuwakombowa wale wote waliokuwa wakidhulumiwa. Hata hivyo kwa mnasaba wa mada hii, Uislamu ulikuja na sharia nyingi zilizolenga kumkombowa mwanamke. Kwa hivyo Aya na Hadithi nyingi zimeteremka kwa lengo la kumrejeshea mwanamke haki zake. Baadhi ya mafunzo hayo ya Uislamu ni pamoja na haya yafuatayo: 

Usawa wa mwanamume na mwanamke katika malezi:

((ساوو بين أولادكم في العطية، فلو كنت مفضلا أحدا لفضلت النساء)) الطبراني 

((Fanyeni usawa baina ya watoto wenu katika upaji/kuwapa, lau ningekuwa wa kumfanya bora mmoja (wao), ningemfanya bora mwanamke)) A-tabrani

((إنما النساء شقائق الرجال)) البراز

((Kwa hakika wanawake ni ndugu (pacha) na wanaume)) Al-buraz

((Yoyote mwenye mtoto wa kike akamlea vyema bila ya kumfadhilisha wa kiume, Mwenyezi Mungu atamuingiza peponi))

((Mwenye kulea watoto wawili wa kike (kwa vyema) mpaka wakakuwa,  siku ya kiama nitakuwa mimi nye kama hivi)) Muslim.

Usawa wa mwanamume na mwanamke katika haki mbalimbali:

Haki hizo ni pamoja na hizi zifuatazo:

i) Haki za kijamii

Sharia ya Kiislamu imemtandikia haki muwafaka mwanamke wa Kiislamu akiwa ni miongoni mwa wanajamii.  Katika hili Sharia inamuangalia mwanamke kama inavyomuangalia mwanamume, hasa katika upande wa haki, majukumu na wajibu. Haya yanabainishwa na Aya ya 134 ya Suratu Nnisaa inayosema: ((Na watakaofanya vitendo vizuri, wakiwa wanaume au wanawake hali wao ni wenye kuamini, basi hao wataingia peponi   wala hawatadhulumiwa hata ugamba wa kokwa ya tende)) Wote ni sawa katika majukumu na haki.  Aya nyengine zinazotilia nguvu kuwepo kwa haki hizo ni pamoja na Surat Nnahli aya 97, – Al-Imran aya 195 na Al-Ahzab aya35.

 Zifuatazo ni baadhi ya nyanja za kijamii ambazo bila ya ubaguzi, Sharia ya Kiislamu imeweka usawa wa haki kati ya mwanamke na mwanamme.

ii) Haki ya uchumi na kumiliki Mali.

Mwenyezi Mungu anasema:

((Wala msitamani vile ambavyo Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu (kwa vitu hivyo) kuliko wengine. Wanaume wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma na wanawake nao wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma. Na mwombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake.  Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu)).   An-nisaa aya 32

Uislamu umempa mwanamke haki ya kumiliki mali na ukamruhusu kuindeleza mali hiyo kwa njia za halali kama kufanya biashara.  Kadhalika ukamuwekea njia za kumiliki mali hiyo kwa kumpa fungu maalumu katika mirathi, kujuzisha kupewa mwanamke zaka, sadaka, hiba na mengine yaliyo halali, (mfano mahari).

Aidha Uislam umeharamisha mwanamke kuchukuliwa mali aliyonayo pasina ridhaa yake kama ilivyokuja katika Suratun Nisaa aya ya 20 na 29, Suratul Baqaraa aya 188.

Pamoja na mwanamke kupewa haki hiyo ya kumiliki mali, Uislamu haujamkalifisha wala kumuwajibisha kutumia mali hiyo kwa kumpa mtu mwengine isipokuwa katika mambo yaliyo ya faradhi, lakini mwenye kuitoa kwa ikhlasi katika njia za kheri kwa khiyari na ridhaa yake ameandaliwa ujira ulio mkubwa kabisa.

Mwanamke wa Kiislamu ana uhuru kamili na haki ya kutafuta, kumiliki na kutumia mali yake apendavyo kulingana na sharia kama ilivyokuja katika Aya ya 32 ya Nnisaa ((…Na wanawake wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma)). Usawa  wa Sharia unajidhihirisha zaidi ulipompa mwanamke uhuru wa kutiliana mikataba na makubaliano ya kibiashara bila ya kuingiliwa na mumewe, baba yake au walii wake.  Zaidi ya haki hizo pia ana uhuru wa kumuwakilisha amtakaye kushughulikia mali yake, kuusia, kugaia na kufanya mengineyo ya halali yanayohusiana na mali kama ilivyo kwa mwanamme.

Kwa upande huu wa kumiliki mali, kuna suala moja linalojitokeza ambalo inabidi pia tuliweke wazi kwa mtazamo wa Sharia ili haki itendeke.  Suala hilo ni haki ya mwanamke katika mali, vifaa au vitu vilivyopatikana wakati wa ndoa.

Ikiwa palikuwa na makubaliano ya tangu awali (ni vizuri yawe ya maandishi) kwamba wanaingia katika asasi ya ndoa na watakachokichuma ni cha ushirika, hapa mwanamke atakuwa na haki ya mali hiyo kwa kiwango waliochokubaliana.

Ikiwa hapakuwa na makubaliano yoyote baina yao, Sharia inampa haki kila mmoja kumiliki kile alichokichuma tu na kuainishwa kwa jina lake.

Ikiwa mwanamke kwa mfano alikuwa akisaidia kuwapikia mafundi wakati nyumba iliyosajiliwa kwa jina la mumewe inajengwa, au akisaidia kwa mengine kama kukubali kujinyima chakula au kulala pazuri lakini hapakuwa na makubaliano yoyote kuwa alipwe au ana haki katika nyumba hiyo, Sharia hailazimishi mwanamke huyo kudai fidia au haki ya hayo aliyoyafanya.  Kufanya hivyo kisharia huitwa hisani ambayo ni vyema pia malipo yake yawe ya hisani.  Vivyo hivyo ikiwa aliyesaidia au aliyetumika ni mwanamme katika nyumba au kazi ya mke. Tunachosisitiza hapa ni umuhimu wa mwanamke kujua haki zake mapema ili kuepusha lawama.  Si vibaya kisharia pakawa na mkataba wa ndoa ambao unaingiza madai na masharti kama hayo.

iii) Haki ya kupata Elimu na Maarifa, na kuyatumia:

Mwanamke wa Kiislamu ana haki na uhuru kamili wa kutafuta elimu na maarifa na kutumia kwa mujibu wa njia za kihalali.  Zipo aya na Hadithi nyingi zinazobainisha hayo.  Moja kati ya hizo ni Hadithi ifuatayo ambapo Mtume (SAW), amesema:  ((Kutafuta elimu ni faradhi (lazima) kwa Muislamu mwanamume na mwanamke)) Bayhaky na Tabaraniy. Pia Mtume (SAW), amesema:  ((Anayeulizwa kuhusu taaluma akaificha, atafungwa kamba za moto siku ya kiama)). Ahmad, Abu Daud, Nasai, Tirmidhy na Ibnu Majah.  Jambo la msingi hapa ni kusoma elimu kwa nia ya ibada.  Nako ni kukusudia kujisaidia mwenyewe, jamii na taifa kimaendeleo katika nyanja zote.

Sharia ya Kiislamu inapomlazimisha mwanamke kusoma na kuifanyia kazi elimu inalenga kwenye elimu za aina zote.  Lakini elimu iliyo bora zaidi kwao ni ile itakayowakomboa kimaarifa na kimaisha.  Hii ni elimu ya kutambua haki na wajibu wao wakiwa kama mama au wake au ndugu wa kike au wanajamii.

Elimu ya pili ni kuleta maendeleo ya jumla.  Sharia haijamkataza mwanamke kufuata elimu popote ilipo. Hadithi ya Mtume (SAW), inasema ((Tafuteni elimu japo Uchina (maeneo ya mbali)). Ibnu Abdulbari, Bayhaqiy n.k. wengine wamesema dhaifu.  Jambo la msingi hapa ni kufuata taratibu za kisharia zinazolinda heshima. Kama kutakuwa na udhamini unaoaminika kisharia mwanamke anaweza kwenda masomoni popote.  Kinachosisitizwa na Sharia ni kwa mwanamke kujua haki na wajibu wake na kufuata taratibu kama hizo za walii.

iv) Haki ya kufanya kazi:

Sharia ya Kiislamu inamhimiza mwanamke kujitahidi kufanya kazi za halali ili apate chumo la halali hasa pale anapokuwa hana mtu anayelazimishwa na Sharia kumhudumia kwa kumtimizia mahitaji yake (kama baba, mume, ndugu wa kiume au walii mwingine n.k). Hata pale wanapokuwapo hao, pia hakatazwi kufanya kazi lakini mhimizo wa hapa si kama ule wa mwanzo.  Mana kule mwanzo unafikia kuwa ni wajibu.

Faida ya elimu tuliyoizungumza hapo juu na ule uhalisia wa kumiliki mali unapatikana na kudhihirika matunda yake kwa kufanya kazi.  vipi utamiliki bila kufanya kazi? Na vipi utafanya kazi kwa mafanikio bila ya maarifa ya kazi hiyo na taaluma yake?  Mtume (SAW), amesema ((Hakika Mwenyezi Mungu anapenda mmoja wenu akifanyakazi aifanye vyema/ kwa ustadi)) Bayhaqiy. Mifano ya Waislamu wanawake wa mwanzo waliofanya kazi ni wengi.  Kazi walizofanya ni pamoja na udaktari, ualimu, ulinzi ukusanyaji kodi n.k.  kwa hivyo Sharia inamruhusu  mwanamke kufanya kazi yoyote ambayo ni ya halali inayoendana na maumbile yake, huku akichunga mipaka mingine ya ibada za maadili, mavazi, heshima na utu unaokubalika katika Sharia.

v) Haki ya kuheshimiwa:

Lengo la Sharia ya Kiislamu ni kuchunga heshima za binaadamu wote pamoja na kulinda haki za viumbe wote. Sharia inatambua vyema na inapigania heshima na utu wa mwanamke katika jamii, hasa kwa kuzingatia jukumu kubwa alilokabidhiwa la kubeba mafanikio ya jamii nzima.  Mwanamke ni nusu ya jamii.  Sharia imempa aula ya juu kabisa.  Ndiyo mana mama amempita baba mara tatu kwa kustahiki heshima ya mtoto.  Zaidi ya hayo Sharia inapozungumzia haki ya kuheshimiwa mwanamke inamaanisha utekelezaji wa hatua maalumuu zinazofikisha kwenye heshima hiyo.  Miongoni mwa hatua hizo inabidi zichukuliwe na zifuatwe na mwanamke mwenyewe, nyengine zitekelezwe na wanaume na nyengine na jamii.  Kwa mnasaba wa kazi hii, tunajaribu kuangalia mambo yafuatayo yatayopelekea heshima na haki ya mwanamke ya kuheshimiwa.

Kujistiri kwa mavazi yanayokubalika na Sharia (Hijabu) Mwenyezi Mungu ameumba kila kitu mbeya mbili mume na mke.  Kila mmoja anavutiwa mno na mwenzake.  Mwenyezi Mungu amewatia jazba ya mapenzi kati yao.  Jazba hiyo ingeachiwa tu bila ya kuwekewa mipaka ingeondosha uwiano wa kibinaadamu na unyama ungetawala.  Hali hiyo ingepelekea kwenye kosa jengine la kukaribia zina au kuzini kabisa, hasa pengine na watoto au na wake za watu.  Heshima ingekuwa imekufa kabisa.

Kwa mantiki hiyo, Sharia ya Kiislamu imefaradhisha sitara ya hijabu kwa mwanamke ili apate heshima zaidi.  Sharia hiyo ilitanguliwa na kukatazwa kuangalia yasiyo halali yanayoamsha mori wa hisia za zina, imeamrisha kustiri tupu na pia kutoregeza sauti au kujiregeza katika mwendo au kufanya jambo lolote litalopekelea kuibua hisia za jinsi na hatimaye kuondosha heshima ya mwanamke na ya jamii.  Katika kuchunga heshima hizo Sharia imeangalia na kuweka mipaka ya namna ya kuchanganyika baina ya wanawake na wanaume. Katika kuchunga heshima na stara ya mwanamke, Mwenyezi Mungu amewaamrisha wote kila mmoja achukue hadhari.  Aya ya 30 na 31 An-nur  ((Waambie Waislamu wanaume wasitizame yaliyokatazwa na wazilinde tupu zao, hili ni takaso (heshima) kwao………)) (( Na waambie Waislamu wanawake wasitizame yaliyokatazwa, na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vinavyodhihirika (uso , vitanga vya mikono – nyayo!) na waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao, na wasionyeshe mapambo yao ila kwa waume zao………………)) Ahzab aya  59.

vi) Kuhifadhiwa Siri.

Sharia ya Kiislamu inasema kuwa “Ukamilifu ni wa Mwenyezi Mungu, Mitume wameepushwa na ufanyaji makosa, watu wa kawaida wanaweza kutahiniwa kwa makosa (au na aibu).  Kuna kauli nyengine ya kisharia isemayo “Binaadamu (wote) wanafanya makosa, na wabora wa wafanayao makosa ni wanaokubali makosa na kutubia”.

Hali ya kumstiri aliyefanya makosa, hasa aliyetubia inapendezeshwa katika Sharia.  Kwa upande mwengine Sharia inaamrisha tuwasiri waliofanya makosa wakatubia, bali pia tuwastiri kuwatolea aibu zao za kimaumbile Mtume (SAW), anasema ((Anayemstiri Muislamu mwenzake atasitiriwa na Mwenyezi Mungu siku ya Kiama)). Bukharina Muslim, Ahmad, Abu Daud, tirmidhiy, Ibnu Majah.

Sharia inahimiza kuhifadhiana siri za ndani ya nyumba (umbo, sura, harufu n.k.).

vii) Haki ya kushirikishwa:

((…Na saidianeni/shirikianeni katika wema na ucha Mungu, wala msishirikiane katika dhambi na uadui …)) Al-Maidah Aya 2

Haki hii ya kusaidiana kimawazo na kifikra na kushauriana kwa kuwashirikisha wanajamii wote wakiwemo wanawake ni katika mahimizo ya Sharia ya Kiislamu.  Jambo la msingi hapa ni kumshirikisha kila mwenye uwezo katika jambo alilo na uwezo nalo.

Katika siku za mwanzo za Sharia ya Kiislamu, wanawake walikuwa wakishirikishwa katika nyanja zote za maisha ikiwemo kazi za ulinzi wa dola, kazi za kuelimisha umma kazi za biashara na nyenginezo.

Uislamu unakataza kabisa kuwatenga watu kwa misingi ya rangi, kabila au jinsi zao.  Mtume (SAW), anasema ((Nyote nyinyi asili yenu inatokana na Adam ambaye anatokana na udongo…..)) Bazar.  Kwa maana hiyo hakuna kumbagua yoyote au kumtenga Muislamu yoyote kwa sababu yeyote.

Haki hii ya kushirikishwa inajumuisha haki nyengine muhimu zikiwemo.

viii) Haki ya kutoa rai na maoni na kusikilizwa 

 Wanawake wa mwanzo katika uislamu walikuwa wakishiriki katika mikutano ya kuchangia maendeleo ya dola na maendeleo yanayohusu sekta ya wanawake hususan.  Katika mkutano mmoja (wa siku ya ijumaa) uliofanyika Msikitini Madina, mwanamke mmoja alisimama na kutoa rai yake ambayo ilikuwa inapingana na rai ya Sayyidna Omar bin Khatab ya kuweka kiwango maalumu cha mahari kwa kila mwanamke.  Kwa maana hiyo Uislamu unathamini rai za kila Muislamu, hasa aliebobea katika fani anayoitolea rai bila ya kuangalia ikiwa ni mwanamke au ni mwanaume.

ix) Haki ya kuthaminiwa na kushauriwa.

  Hii ni amri iliyokuja katika.  Mwenyezi Mungu anasema ((…Na wanashauriana katika mambo yao…)) Ash-Shuura aya 38. Kwa mantiki hii, mwanamke ana haki ya kushauriwa na kuthaminiwa maoni yake katika mambo yote yanayomhusu binafsi, jamii na taifa zima.  Ni lazima ashauriwe katika mambo yote yanayohusu uendeshaji wa nyumba zao, watoto wao na waume wao.  pia wana haki ya kushauriwa katika mambo yanyohusu mustakbali wa nchi yao. Mwenyezi Mungu anasema ((…Na ushauriane nao katika mambo)). Al -Imran Aya 159

x) Haki ya kuishi na kuwa hai:

Sharia ya Kiislamu inautaja uhai kuwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.  Ni haki ya mtu itokayo kwa muumbaji.  Kwa hivyo hakuna yoyote mwenye ruhusa ya kuondosha uhai wa mwengine kimwili au kiakili.  Amri hii imekuwa inalindwa zaidi kwa wanawake ambao kihistoria walikuwa wakinyimwa uhai wao kabla ya Uislamu. 

Ni haramu kujitoa roho, kujinyonga na kudhulumiwa uhai kwa sababu yoyote iwayo isipokuwa ya kisharia. Mwenyezi Mungu anasema ((…Wala msijiue wala msiue wenzenu…)). Annisaa aya 29. Kwa hivyo haifai kumtesa mwanamke, kumpiga, kumjeruhi, kumpoozesha au kumtia maradhi.

xi) Haki ya kufurahia maisha/uhai:

Sharia ya Kiislamu imefungamanisha haki ya kuishi na haki ya kufurahia maisha. Mwenyezi Mungu anasema. ((…Sema:  Ni nani aliyeharamisha (aliyekataza) mapambo ya Mwenyezi Mungu ambayo amewatolea waja wake. Na nani aliyeharamisha vitu vizuri katika vyakula?  Sema: “Vitu hivyo vimewahalalikia Waislamu hapa katika maisha ya dunia na vitakuwa vyao peke yao siku ya Kiama)). Al-Aaraf aya 32

Mwanamke kama mwanamme anatakiwa aifanyie kazi dunia kama ataishi milele.  Pia Mwenyezi Mungu anapenda amuone mwanamke anatumia riziki alizompa vizuri na kwa manufaa ya dunia yake na akhera.  Kwa hivyo hapana sharia inayoruhusu kumzuilia mwanamke starehe za halali zisizopingana na mwenendo wa uislamu.

xii) Haki ya Uhuru wa Kuamini:

Binaadamu wote akiwemo mwanamke wameumbwa na Mwenyezi Mungu na akapewa akili na uwezo wa kupambanua mema na mabaya.  Ameoneshwa njia na kaachiwa uteuzi. Mwenyezi Mungu anasema ((Kwa hakika tumemuumba mtu kutokana na mbegu za uhai, zilizochanganyika ili tumfanyie mitihani. Kwa hivyo tukamfanya ni mwenye kusikia na mwenye kuona.  Hakika sisi tumemuongoa/tumembainishia njia mbili ya kheri na ya shari.  Basi yeye mwenyewe tena atakuwa mwenye shukurani au mwenye kukanush)) Addahar aya 2-3.

Kwa hivyo mwanamke asilazimishwe kuwa lazima afuate kundi fulani ikiwa la mumewe la baba yake au la viongozi.  Mwenyezi Mungu anasema: ((Hakuna kulazimishwa mtu kuingia katika dini (imani)) Albaqarah aya 256. Mwenyezi Mungu angetaka dunia nzima ingekuwa katika Uislamu.

xiii) Haki ya kuwa na maoni tofauti:

Sharia ya Kiislamu inabainisha kwamba kuwapo kwa tofauti ya mambo duniani ni katika kufanikisha raha na maslahi ya dunia.  Kwa hivyo rangi, kabila, mawazo na tafauti ya maoni ni mambo yaliyoletwa na Mungu ili kuthibitisha kuwapo kwake na kwa lengo la kunufaisha wanadamu.  Mwanamke anaruhusiwa kwa hivyo, na ni haki yake atowe maoni yake japo yanatafautiana na walio na mamlaka kwake.  Mwenyezi Mungu anasema: ((Na kila (umma) kati yenu binaadamu tumejaalia sharia yake na njia yake)) Almaida aya 48. Siyo dhambi kwa mwanamke kuwa na maoni yake juu ya maendeleo. La msingi ni kuwa na dhamira iliyo ndani ya misingi ya Uislamu.

xiv) Haki ya Usawa (wa Kijamii)

 Mwenyezi Mungu anasema: ((Enyi watu! Kwa hakika tumekuumbeni nyote kwa yule yule mwanamume mmoja na yule yule mwanamke mmoja………… Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi)). Al-hujraat aya 13

Kwa mantiki ya aya hiyo, watu wote kiasili ni sawa katika ubinaadamu wao, tafauti yao itakuwa mbele ya Mungu katika uchaji.  Hakuna mbora kwa kabila, jimbo, nasaba au jinsi.  Hata hivyo katika upande wa kibaiolojia zipo tofauti za kimaumbile ambazo zikiheshimiwa na kuthaminiwa ndipo ule usawa wa asili wa kijamii hufanyakazi, Sharia inakataza kumdhalilisha mwanamke kutokana na misingi yoyote ikiwemo ile ya kijinsi.

xv) Haki ya kufanyiwa Uadilifu:

Mwenyezi Mungu anasema:  ((Kwa hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu na kufanya hisani……)) Annahl aya 90

Sharia ya Kiislamu hapa inawataka wanajamii wafanyiane uadilifu wakati wote. Wanapotoa ushahidi au hata wanapohukumu.  Kwa hivyo kuwasingizia baadhi ya wanawake kuwa wazinzi au kuwatupia sifa mbaya si uadilifu.  Pia kuwa na mke zaidi ya mmoja na akafadhilishwa na kupendelewa mmoja si uadilifu. Vile vile kuwa na watoto wa kike na wa kiume wakafadhilishwa na kupendelewa wa kiume inavunja uadilifu.

Hiyo ni mifano tu ya haki mbali mbali ambazo mwanamke wa Kiislamu amepewa na Uislamu ambapo katika tamaduni nyengine zinakosekana.

Makala hii imeandaliwa na Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Dk Issa Haji Ziddy.

Advertisements

11 Replies to “MAKALA”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s