MAPISHI


 MAPISHI YA MWAMBAO VYAKULA VIKUU

BSHHH

 

WALI WA ASUMINI

 

Mchele kilo 1

Kuku mkubwa 1

Vitunguu maji kilo 2

Mayai 8

Samli kilo 1

Thomu gram 200

Tangawizi mbichi gram 50

Mdalasini gram 50

Hiliki gram 50

Bizari nzima kiasi

Siki kiasi

Mtindi painti 1

Tungule kilo 1

Zabibu nyeusi kiasi

1                    Mkate kuku umwoshe umchemshe kwa maji na chumvi mpaka awive, kisha muepue.

2                    Menya vitunguu uvioshe uvikate na uvigawe sehemu mbili. Sehemu moja uiweke, sehemu ya pili vikaange mpaka viwe vyekundu kama vya biriani. Kisha vichuje uitoe samli yote, vitie katika sinia uvitandaze ili vipoe kwa kupata upepo.

3                    Chukua mdalasini, hiliki na bizari utwange pamoja, kisha uchunge unga laini. Saga thomu na tangawizi mbichi. Saga tungule.

4                    Teleka sufuria tia samli ile ile iliyokaangiwa vitunguu halafu utie vile vitunguu vilivyobakia uvikaange. Vikianza kuiva tia viungo ulivyovitwanga na kuvisaga. (Bakisha vitunguu na viungo kidogo). Tia vipande vya kuku, mtindi  siki na supu ya kuku iliyobakia katika sufuria. Acha ichemke nyama pamoja na vitu vyote  mpaka libaki rojorojo.

5                    Teleka maji, yakichemka tia chele. Ukiiva utoe uchuje yatoke maji yote.

6                    Teleka tena sufuria utie samli kidogo utie na vile vitunguu ulivyovibakisha uvikaange. Tia mdalasini nzima, kaanga pamoja, tia na ule wali ukoroge koroge ili uchanganyike na viungo. Kisha ufunike upalie moto.

7                    Chemsha mayai yote uyamenye.

8                    Wali ukishakauka utaupakua, lakini lazima itabidi utumie kombe au sahani kubwa itakayoweza kuingia wali pamoja na vitu vyote. Kuupakua kwake kwanza utatia nusu ya wali katika hiyo sahani, baadae utatia masalo na nyama yote, na mayai, kisha utayafunika masalo kwa wali uliobakia. Mwisho utachukua vile vitunguu ulivyovikaanga na ukavitandaza ili vipo, utavimwaga juu ya wali.Kwani ni kwa sababu ya hivi vitunguu ndio maana ukaitwa wali wa asumini. Ukipenda utapamba chembe za zabibu juu yake. ZABIBU HIZO Ziroweke kwanza ili zivimbe.

 

WALI WA BIRIANI

 

Mchele kilo 1

Nyama kilo 1

Samli ½ kilo 

Mbatata ½ kilo 

Vitunguu maji kilo 1

Thomu gram 150

Tangawizi mbichi gram 150

Hiliki gram 50

Mdalasini gram 100

Mtindi painti 1

Siki kiasi

Majani ya nanaa fungu moja

Chumvi kiasi

Zaafarani kidogo (irowekwe kwa maji ya moto nusu kikombe cha kahawa)

Tungule ilosagwa

Tungule ya kopo

1                    Menya vitunguu maji uvioshe uvikate. teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange bila ya kuvivuruga mpaka viwe vyekundu. Vichuje uvitoe halafu vitandaze katika sinia.

2                    Twanga mdalasini na hiliki mpaka viwe laini kama unga. Menya thomu uitwange pamoja na tangawizi mbichi.

3                    Kata nyama vipande vikubwa kisha tia chumvi na vitu ulivyovisaga (yaani tangawizi mbichi na thomu) vile vile tia unga unga wa mdalasini na hiliki pamoja na mtindi wa maji. Pika mpaka karibu nyama kuiva kabisa ndipo utie mbatata. Ukiona mbatata zimeshaiva tia siki.Usiache kukauka kabisa, bakiza rojorojo. Tia maji katika sufuria na chumvi yakichemka tia mchele. Acha utokote, angalia kiini cha wali ukiona umeshaiva uchuje.

4                    Angalia sufuria ya nyama na rojo lake lisiwe limekauka kabisa, lazima ziwe na maji kidogo. Chukua vile vitunguu ulivyovikaanga vikapoa uvinyunyuzie juu ya masalo yote (usikoroge). Halafu utie mchele uliouchuja, nyunyuzia maji ya zaafarani juu ya wali wote halafu unyunyuzie samli ile uliyochuja kutoka kwenye vitunguu ulivyovikaanga ienee juu ya wali wote. Kisha funika upalie makaa.

5                    Wali ukishakuwa tayari utaupakua. lakini unapotaka kuupakua lazima kwanza uutoe wali wote mweupe uutie katika chombo chengine, halafu uyakoroge masalo yachanganyike sawasawa kisha ndio uyatie juu ya wali katika kila sahani.

 

BIRIANI YA SAMAKI

 

Mchele kilo 1

Samaki kilo 1

Vitunguu kilo 1

Samli ¾ kilo

Thomu kiasi

Mdalasini kiasi

Hiliki kiasi

Ndimu kiasi

Tungule kiasi

Chumvi kiasi

1                    Mkate kate samaki umtie chumvi na ndimu umkaange. menya vitunguu uvikate. saga tungule, thomu na viungo vyote vilivyobakia. (Bakisha mdalasini nzima kidogo).

2                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange, vikianza kupiga wekundu tia tungule na viungo kidogo. Acha vikaangike kwa muda mdogo halafu tia vipande vya samaki, chumvi na ndimu, pamoja na maji kidogo. Acha ichemke kwa muda mdogo. Likibaki rojorojo epua.

3                    Chukua sufuria jengine uitie maji na chumvi. yakichemka osha mchele utie. acha utokote. Angalia kiini cha wali, ukiona umeshaiva umimine uyachuje maji yote. Teleka tena sufuria utie samli kidogo, ikichemka tia vitunguu kidogo pamoja na vile vilivyobakia.Vyote vikaange kidogo halafu umimine wali wote ukoroge koroge ili upate kuchanganyika na viungo. Halafu uweke vizuri upalie moto. Ukishakauka utaupakua. Kuupakua kwake kwanza utatia wali kwenye sahani, baadae ndio utatia samaki pamoja na rojo rojo lake lote kwa juu.

 

WALI WA PILAU

 

Mchele kilo 1

Nyama kilo 1

Samli ¼ kilo

Vitunguu maji ½ kilo

Vitunguu thomu gram 100

Tangawizi mbichi gram 100

Mdalasini gram 50

Hiliki gram 25

Pilipili manga gram 100

Zabibu gram 100

Chumvi kiasi

1                    Teleka nyama utie chumvi na maji uipike mpaka iive. Baadae epua uiweke (ubakishe supu itakayotosha kuweza kuivisha mchele).

2                    Menya vitunguu uvikate. Menya vitunguu thomu na tangawizi mbichi utwange pamoja. Menya hiliki uitwange pamoja na bizari nzima. osha vijiti vya mdalasini pamoja na chembe za pilipilimanga uziweke. Osha zabibu uziweke. Menya mbatata uzioshe uziweke.

3                    Teleka sufuria tia samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Tia thomu na tangawizi mbichi uliyoisaga tia vipande vyote vya nyama bila supu, tia mbatata na viungo vyote ulivyovisaga na kuviosha, isipokuwa zabibu. Kaanga kwa muda mfupi, baadae tia supu yote. Ikianza kuchemka tia mchele, onja chumvi. Angalia kiini cha mchele, ukiona wali umeiva na kukauka, fukua kati utie zabibu zote na baadae funika upalie moto.

 

PILAU YA PAPA MKAVU

 

Mchele kilo 1

Papa mkavu kilo 1

Vitunguu ½ kilo

Samli ¼ kilo

Bizari nzima kiasi

Thomu kiasi

Mdalasini kiasi

Hiliki kiasi

Chumvi kiasi

1                    Mkatekate papa umuoshe umchemshe, halafu umuoshe tena atoke mchanga wote, kisha mueke.  Kata vitunguu, saga thomu, hiliki na bizari nzima.

2                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Vikianza kupiga wekundu tia thomu pamoja na viungo vyote vilivyobakia ukaange kidogo kisha tia maji na chumvi. Acha yachemke kisha tia mchele. Acha uchemke mpaka yakauke maji yote. Fukua kati umtie papa wote halafu upalie moto.

3                    Wali ukishakauka utaupakua kwa upole bila ya kumvuruga papa.

 

WALI WA CHOOKO

 

Mchele kilo1

Chooko ½ kilo

Samli kiasi

Nazi 2 nzuri

Vitunguu thomu kiasi

Bizari nzima kiasi

Vitunguu maji kiasi

Hiliki kiasi

Mdalasini kiasi

Chumvi kiasi

Karafuu chembe 2 au 3

1                    Osha mchele pamoja na chooko uweke pembeni.

2                    Kuna nazi uchuje tui kama la wali wa nazi uliweke.

3                    Menya vitunguu maji, uvioshe uvikate uviweke. Menya vitunguu thomu uvitwange pamoja na bizari na hiliki. Osha vijti vya mdalasini na chembe za karafuu uziweke.

4                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Baadae tia viungo vyote ulivyovitwanga utie na chembe za karafuu pamoja na vijiti vya mdalasini. Kisha tia tui la nazi. Likianza kufumba tia mchele pamoja na chooko zake utie na chumvi. Acha utokote mpaka wali ukauke. Ukishakauka funika upalie moto.

 

BIRIANI YA KUKU

 

Mchele kilo 1

Kuku mkubwa 1

Samli ½ kilo

Mbatata ½ kilo

Vitunguu maji kilo 1

Thomu gram 150

Tangawizi mbichi gram 150

Hiliki gram 50

Mdalasini gram 100

Mtindi painti 1

Siki kiasi

Chumvi kiasi

Zaafarani kiasi (iroweke katika maji ya moto nusu kikombe cha kahawa)

1                    Meya vitunguu maji uvioshe uvikate. teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange mpaka viwe vyekundu. Vichuje utoe samli yote kisha vitandaze vipate kupoa.

2                    Twanga mdalasini na hiliki viwe laini, menya thomu na tangawizi utwange pamoja.

3                    Mkatekate kuku umtie chumvi, mtindi, thomu, tangawizi, na unga wa hiliki na mdalasini, na umpike.(Akiwa mgumu sana tia maji kidogo). Kisha tia siki umpike mpaka aive na abaki rojo rojo. Chemsha mbatata mbali kisha uzitie.

4                    Teleka sufuria nyengine utie maji na chumvi, yakichemka tia mchele. Angalia kiini cha wali, ukiona umeshaiva umimine katika chujiouchuje maji yote.

5                    Angalia sufuria yenye kuku isiwe imekauka, lazima iwe na rojo rojo. Iweke tena juu ya moto, uchukue vile vitunguu ulivyovitandaza vipoe uvinyunyizie  vyote juu ya masalo ya kuku. Kisha utie wali wote juu yake. Chukua maji ya zaafarani utie kwa juu na utie samli yote uliyoichuja kwenye vitunguu. Kisha funika upalie moto. Wali ukishakauka utaupakua kwenye sahani kisha utamweka kuku na masalo yote juu yake. 

 

PILAU YA KUKU

 

Mchele kilo 1

Kuku mkubwa 1

Samli ¼ kilo

Vitunguu ½ kilo

Thomu gram 100

Tangawizi mbichi gram 100

Mdalasini gram 50

Hiliki gram 50

Bizari nzima gram 25

Zabibu gram 100

Pilipili manga kiasi

Chumvi kiasi

1                    Mkate kuku umpike kwa maji na chumvi mpaka aive. wakati wa kumuepua angalia kuwa ana supu itakayotosha kuivisha mchele.

2                    Menya vitunguu uvioshe na kuvikata pamoja. Menya thomu na tangawizi mbichi pamoja. Twanga bizari nzima na hiliki. Osha vijiti vya mdalasini na chembe za pilipili manga uweke kando.

3                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Vikianza kupiga wekundu tia thomu na tangawizi mbichi pamoja na viungo vyote vilivyobakia. Kaanga kidogo kisha tia mbatata na vipande vya kuku na umimine supu yote. Ikianza kuchemka tia mchele. Acha utokote. Onja chumvi.Angalia, ukiona wali umeshakauka fukua kati utie zabibu kisha palia moto.Wali ukishakauka utaupakua. kama unavyopakua wali wa pilau na nyama.

BOKOBOKO

Ngano nzima kilo 1

Nyama kilo 2

Mchele ¼ kilo

Samli ½ kilo

Vitunguu kiasi

Thomu kiasi

Bizari nzima kiasi

Hiliki kiasi

Mdalasini kiasi

Giligilani kiasi

1                    Teleka ngano na nyama na maji upike mpaka viive viwe laini sana. Osha mchele utie. Saga vitunguu pamoja na viungo vyote uvitie na uendelee kuvipika vyote pamoja huku unavikoroga mpaka vichanganyike na viive vyote na maji yote yakauke. (Unaweza kutia chumvi kidogo ukipenda). Funika upalie moto.

2                    Utakapokauka funua uanze kulisonga bokoboko. Lisonge mpaka lishikane sawasawa halafu liipue.

3                    Chukua samli uichemshe pamoja na hiliki kisha kila unapopakua utakuwa unalilazalaza na kulitengeneza kwa samli. Wengine hupenda kutengeneza kishimo kati kati yake na kukijaza samli ya moto. Watu wengine hupenda kulila tupu,  na wengine hula kwa sukari au kwa mchuzi wake ambapo hutengenezwa mahsusi.

 

 

MCHUZI WA BOKO BOKO

 

Tende au zabibu kilo1

Samli ¼ kilo

Vitunguu kiasi

Thomu kiasi

Giligilani kiasi

Bizari nzima kiasi

Siki kiasi

Hiliki kiasi

Sukari kiasi

1                    Ziroweke zabibu ndani ya maji kisha uzifikiche mpaka zilainike (usizikamue ukayatoa masimbi yake). Kama ni tende, zitoe kokwa uzikande na kuzivuruga kwa maji. menya vitunguu uvikate. Menya thomu usage pamoja na viungo vyote.

2                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Vikianza kupiga wekundu tia viungo vyote, ukaange. Kisha tia zabibu au tende na sukari na siki. Ikiwa maji uliyorowekea tende ni kidogo, ongeza mengine kidogo. Acha ichemke kisaha epua.

NDIZI MBIVU

Ndizi mbivu za kupika 10

Nazi kavu 3

Sukari kiasi

Hiliki kiasi

1                    Zipasue ndizi katikati kwa marefu, uzitoe moyo wake.

2                    Zimenye kisha maganda uyaoshe. Yapange vizuri maganda hayo ndani ya sufuria safi (kwa chini). Chukua vipande vya ndizi uvipange juu ya maganda.(ndizi ziweke chali, usizifudikize).

3                    Kuna nazi uchuje tui zito mbali na jepesi mbali. Chukua tui jepesi ulitie katika ndizi kisha uziteleke. Zipike mpaka tui likauke na ndizi ziive. Nyunyuzia sukari kidogo. Twanga hiliki utie juu yake. Chukua lile tui zito ulimimine uache liwe linatokota kwa moto mdogo sana. Tui likikauka na kutoa mafuta epua na uziache zipoe. Unapopakua, zitoe taratibu bila ya kuzivuruga.

 

NDIZI MBICHI

Ndizi 15 au 20

Nazi kavu 2

Vitunguu kiasi

Thomu kiasi

Ndimu kiasi

1                    Zimenye ndizi uzipare na utoe utomvu wote. Zikate vipande vipande. teleka sufuria utie maji ya kiasi cha kuivisha ndizi.

2                    Kuna nazi uchuje tui zito mbali na jepesi mbali. Menya vitunguu uvikate. saga thomu.

3                    Maji yakikauka tia vitunguu, chumvi na thomu pamoja na tui jepesi. Acha litokote mpaka tui lote jepesi likauke. Mwisho tia ndimu kidogo ukipenda, utie na tui zito. Acha zitokote mpaka karibu na kukauka ndipo uepue.

TAMBI ZA NAZI

Tambi kilo 1

Sukari ¼ kilo

Nazi kavu 2

Hiliki kiasi

Arki kiasi

1                    Teleka maji, yakichemka zitie tambi zichemke kidogo, kisha zimimine katikachujio au kumto yatoke maji yote.

2                    Kuna nazi uchuje tui zito. Menya hiliki utwange utie katika tui.

3                    Liteleke tui ulipike na huku unalikoroga, kisha tia tambi utie na sukari uwe unazigeuzageuza kwa mwiko mpaka tui lote likauke lianze kutoa mafuta.

4                    Ziepue uache zipoe. baadae zipakue.

TAMBI ZA KUKAANGA

Tambi kilo 1

Sukari ¼ kilo

Samli ¼ kilo

Hiliki kiasi

Arki kiasi

Zabibu (zioshe uziroweke kidogo kwenye maji ya moto).

1                    Zichukue tambi uzivunjevunje katika sinia au ungo.

2                    Teleka sufuria juu ya moto utie samli. Ikichemka tia tambi zote uwe unazikaanga mpaka zipige wekundu. Tia sukari, hiliki au arki pamoja na maji ya moto. Acha zichemke mpaka uone kiini cha tambi kisiwe laini sana na maji yote yakauke.

3                    Ziepue uache zipoe kidogo. Baadae zimimine kwenye sahani. chukua zabibu upambie juu yake.

VIPOPOO VYA UWANGA

Uwanga ½ kilo

Sukari kilo 1

Nazi 6

Hiliki kiasi

Arki kiasi

1                    Uchunge uwanga uwe safi sana. Kuna nazi uchuje tui zito mbali na jepesi mbali. Menya hiliki uitwange.

2                    Ukande uwanga kwa maji ya moto uufinyange donge. Katakata madonge madogo madogo halafu uyasokote. Baadae ukate vipopoo vidogo vidogo, kama chembe za mbaazi au hata vidogo kuliko hivyo.

3                    Teleka sufuria utie maji, yakichemka vitie hivyo vipopoo vyote uache vichemke kidogo halafu vimimine kwa haraka katika chujio yatoke maji yote.

4                    Teleka tena sufuria utie tui jepesi, sukari, arki na hiliki upike na huku unakoroga. Tui likianza kuchemka, vitie vipopoo vyote uwe unavikoroga mpaka viwe vimeshakauka vizito vya kiasi viepue. Kupakua kwake tafuta sahani ndogo ndogo za shimo au vibakuli vidogo vidogo uvitie na baadae uviweke kwenye upepo vipate kuganda.

 MAPISHI YA MWAMBAO  VITOEO

HHH

 

KUKU WA KUPAKA

 

Kuku mkubwa 1

Nazi nzuri 2

Tungule kubwa 2

Vitunguu kiasi

Limau kiasi

Chumvi kiasi

Vitunguu thomu kiasi

Hiliki kiasi

1                      Mteleke kuku ndani ya sufuria yenye nafasi bila ya kumkata. Mtie chumvi, limau na maji kidogo umpike mpaka akaukie na aive.

2                      Menya vitunguu uvisage. Menya vitunguu thomu na hiliki usage pamoja. Menya tungule uzisage.

3                      Kuna nazi uchuje tui zito kisha uvitie vitu vyote ulivyovisaga ndani ya tui. Lipike na huku unalikoroga mpaka liwe zito na lishikane.

4                      Mchukue kuku umtumbukize ndani ya tui uwe unamgeuza geuza mpaka tui likauke lianze kutoa mafuta.

5                      Toa moto wote ubakie vuguvugu, kisha mfunike umpalie makaa kidogo. Baada ya muda mfupi mfunue umtie kwenye sahani, kisha utoe tui lote lililobaki kwenye sufuria ulipake juu ya kuku.

 

KUKU WA KUIKIZA

 

Kuku mkubwa 1 

Vitunguu kilo 1

Samli kilo 1

Tungule kilo 1

Mayai 8

Vitunguu thomu kiasi

Bizari kiasi

Hiliki kiasi

Limau kiasi

Chumvi kiasi

Pilipili manga kiasi

1                    Mkate kuku umchemshe kwa maji, chumvi na limau, thomu pamoja na vitunguu kidogo mpaka aive na akaukie.

2                    Teleka sufuria utie samli. kaanga vitungu mpaka viwe manjano. Menya tungule uzisage. Saga thomu, hiliki bizari na pilipili manga utie vyote katika vitunguu ukaange pamoja mpaka liwe rojo jekundu zito zito.

3                    Teleka legeni kwenye moto mdogo utie rojo nusu yake katika legeni kisha mtoe kuku mifupa bila ya kumvuruga uie hiyo nyama ya kuku kwenye lile rojo kisha utie lile rojo lililobakia. Baadae vunja mayai uwe unayatia kwa upole bila ya kuharibu viini vyake. vipange viini kwa mpango mzuri.

4                    Funika kwa mkungu upalie moto mdogo mdogo ili viini vya mayai viive vizuri bila ya kuungua. funua, ukiona tayari pakua kwa utaratibu utie kwenye sahani bila kuharibu.

KUKU WA DENGU

 

Kuku 1 mkubwa

Vitunguu ½ kilo

Dengu ½ kilo

Samli ½ kilo

Mtindi ½ painti

Ndimu kiasi

Thomu kiasi

Bizari nzima kiasi

Tungule kiasi

Hiliki kiasi

Mdalasini kiasi

Zabibu nyeusi kiasi

Zaafarani kidogo (iroweke)

1                    Mchemshe kuku bila ya kumkata umtie ndimu na chumvi mpaka akaukie. Chemsha dengu ziweke.

2                    Menya vitunguu uvikate. Menya thomu usage pamoja na hiliki na mdalasini. Menya tungule uzisage.

3                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia tia vitunguu uvikaange. Vikianza kupiga wekundu tia tungule ukaange, tia vitu vyote ulivyosaga, tia zabibu na ukaange kidogo, kisha mtie kuku mzima mzima pamoja na dengu.

4                    Tia ndimu na chumvi kidogo uonje. Ukiona kila kitu sawa mgeuzegeuze kuku kwenye viungo mpaka vimwingie kila mahali, kisha mtoe umtie kwenye sahani.

 

KUKU WA MAHSHAI AU KUKU WA KUJAZA

 

Kuku 1 mkubwa

Mchele ½ kilo

Vitunguu ½ kilo

Samli ½ kilo

Thomu kiasi

Bizari nzima kiasi

Tungule kiasi

Hiliki kiasi

Zabibu kiasi

Chumvi kiasi

1                    Bila ya kumkata, mchemshe kuku kwa maji na chumvi. Kata vitunguu, saga thomu na viungo vyote uvitie vichemke pamoja mpaka ukaukie (bakiza viungo kidogo).

2                    Tia samli katika sufuria umtie kuku na kumkaanga mpaka awe mwekundu. Kisha muepue.

3                    Teleka sufuria utie vitunguu kidogo pamoja na viungo vilivyobakia  uvikaage. Chemsha mchele kisha uuchuje uutoe maji yote na baadae uutie katika ile sufuria yenye viungo ukoroge  pamoja mpaka ukauke. Fukua kidogo utie zabibu kisha upalie moto kama wali wa pilau. Ukishakauka wali upakue uujaze katika tumbo la kuku na umshikize kwa uzi mwembamba (yaani umshone) ili ule wali usitoke. Kisha mtie kwenye sahani.

 

 

KUKU WA KUKAUSHA

 

Kuku 1 mkubwa

Vitunguu ¼ kilo

Nazi 2

Tungule ¼ kilo

Pilipili mbichi 3 au 4

Chumvi kiasi

Thomu kiasi

Hiliki kiasi

Ndimu kiasi

1                    Mkate kuku umwoshe umtie chumvi na ndimu. Saga thomu na hiliki utie. Kata tungule utie. Pika mpaka awive na akauke.

2                    Kuna nazi uchuje tui zito utie, uache litokote pamoja na kuku mpaka litoe mafuta na likauke kabisa. Kisha epua.

 

KUKU WA KUCHOMA NA WA KUKAANGA

 

Kuku mkubwa 1

Thomu kiasi

Tangawizi mbichi kiasi

Pilipili  manga kiasi

Ndimu 2

Chumvi kiasi

1                    Mkate kuku vipande vipande umsugulie chumvi na umkamulie ndimu. Twanga thomu, tangawizi na pilipili manga umsugulie. Kisha muweke ili aregee.

2                    Washa moto wa makaa kisha uweke uma uwe unamchoma kama vile unavyochoma mishikaki.

3                    Kadhalika kuku wa kukaanga ni hivi hivi isipokuwa badala ya kumchoma unamkaanga katika mafuta.

  

SAMAKI WA KUPAKA

 

Samaki mkubwa i

Nazi 3

Vitunguu ¼ kilo

Thomu kiasi

Hiliki kiasi

Pilipili mbichi kiasi

Ndimu kiasi

Tungule kiasi

Chumvi kiasi

1                    Mwoshe samaki umtie misingi kisha umsagie pilipili na chumvi na umkamulie ndimu kidogo kisha umtie katika kijiti au mbano. Mchome kwa moto mdogo aive.

2                    Kuna nazi uchuje tui ziti zito. Saga vitunguu, tungule, thomu na hiliki.

3                    Teleka tui juu ya moto utie vitunguu pamoja na vitu vyote ulivyovisaga utie chumvi na ndimu. Lipike tui pamoja na vituvyote hivyo kwa kulikoroga bila kusita mpaka likauke lianze kutoa mafuta.

4                    Mchukue samaki uwe unampaka tui kidogo kidogo na huku unamchoma mpaka tui limuingie sawasawa.

5                    Mtoe samaki katika kijiti au mbano umweke katika kombe lenye nafasi kisha uchukue tui lote lililobakia ulipake juu ya samaki.

 

SAMAKI WA MAYAI

 

Samaki  (nguru)  kilo1

Vitunguu kilo 1

Tungule kilo 1

Samli ½ kilo

Mayai 6

Thomu kiasi

Pilipili manga kiasi

Bizari nzima kiasi

Ndimu kiasi

Chumvi kiasi

1                    Mkatekate samaki umtie chumvi, pilipili na ndimu umkaange kisha mtoe umuweke.

2                    Kata vitunguu, saga tungule, thomu na viungo vyote vilivyobakia.

3                    Teleka sufuria utie samli. Ikichemka tia vitunguu uvikaange mpaka vipige wekundu. Tia tungule, thomu pampja na viungo vyote. CHUKUA VIPANDE Vyote vya samaki uvitie, kisha tia ndimu na maji kidogo. Kisha onja, ukiona kila kitu sawa vunja mayai moja baada ya jengine uwe unayaweka juu ya samaki kwa mpango mzuri bila ya kuharibu viini vyake.Funika kwa mkungu upalie moto mdogo mdogo juu yake ili mayai yapate kuiva.

4                    Angalia, ukiona epua upakue kwa upole bila ya kuharibu mpango wa mayai.

 

SAMAKI WA ROJO

 

Samaki mkubwa 1

Vitunguu kilo 1

Tungule kilo 1

Samli ½ kilo

Pilipili manga kiasi

Thomu kiasi

Ndimu au ukwaju kiasi

Bizari nzima kiasi

Chumvi kiasi

1                    Mwoshe samaki (usimkate) umtie pilipili, chumvi na ndimu.

2                    Kata vitunguu, saga thomu, tungule pamoja na viungo vyote vilivyobakia.

3                    Teleka chuma utie samli. ikichemka mtie samaki umkaange vizuri mpaka aive. Mtoe umtie katika kombe au sahani kubwa ya shimo.

4                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia viunguu uvikaange mpaka vipige wekundu. Tia tungule na viungo vyote. Tia chumvi, ndimu na maji kidogo. Wacha ichemke mpaka ikauke. Chukua rojo lote umimine juu ya samaki lakini kwa utaratibu, umfunike samaki wote kwa rojo.

 

SAMAKI WA KUKAUSHA

 

Samaki kilo 1

Vitunguu ½ kilo

Tungule ½ kilo

Nazi 2

Pilipili mbichi chembe 4

Ndimu kiasi

Chumvi kiasi

1                    Mkate samaki vipande vipande umsagie chumvi na pilipili na umkamulie ndimu. Menya vitunguu uvikate, katakata tungule ukaushe vyote pamoja na samaki mpaka akaukie.

2                    Kuna nazi uchuje tui zito utie juu yake upike mpaka likauke kabisa wala usikoroge. Akishakauka epua umpakue vizuri bila ya kumvuruga.

 

NYAMA YA KUIKIZA

 

Nyama iliyosagwa kilo 1

Vitunguu ½ kilo

Tungule ½ kilo

Samli ¼ kilo

Thomu kiasi

Bizari nzima kiasi

Tangawizi mbichi kiasi

Pilipili manga kiasi

Limau kiasi

Mayai 6

Chumvi kiasi

Mbatata ½ kilo

1                    Osha nyama uiweke katika chujio ivuje maji yote.

2                    Kata vitunguu, menya mbatata ukate nyembamba, saga tungule, thomu na viungo vyote vilivyobakia.

3                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange mpaka vipige wekundu. Tia tungule pamoja na mbatata na viungo vyote vilivyobakia. Baadae tia nyama ukaange. Tia chumvi, limau na maji kidogo. Acha ichemke mpaka ikauke, kisha epua, tafuta legeni la kiasi umimine nyama yote uiweke vizuri kama mkate, halafu vunja mayai moja baada ya jengine uyapange vizuri juu ya nyama bila ya kuharibu viini. Ukishayatia mayai yote funika kwa mkungu upalie moto juu yake, lakini usiwe moto mkali, moto uwe mdogo ili usiunguze viini.

 

MBOGA YA MCHICHA NA NAZI

 

Mchicha mafungu 3 makubwa

Nazi 3

Tungule ½ kilo

Vitunguu ½ kilo

Chumvi kiasi

Hiliki kiasi

1                    Uchambue mchicha uuoshe vizuri kisha uuteleke uupike kwa maji kidogo mpaka uive.

2                    Kuna nazi uchuje tui zito zito. Kata vitunguu, menya tungule, na umenye hiliki na uzitwange.

3                    Maji yakishakauka tia vitunguu, tungule na chumvi, utie na yui lote upike mpaka tui likauke, kisha epua.

 

MBOGA YA MAJIMBI AU MAYUGWA

 

Mayugwa fungu 1 kubwa

Nazi 2

Vitunguu ½ kilo

Tungule ½ kilo

Chumvi kiasi

Hiliki kiasi

1                    Ichambue mboga uitoe nyuzi kisha uikate kate na uichemshe.

2                    Kuna nazi uchuje tui zito zito. Saga vitunguu, saga tungule na usage hiliki.

3                    Maji yakishakauka isagesage mboga mpaka iwe laini, kisha tia vitunguu, tungule, hiliki na chumvi. Baadae tia tui upike mpaka ikaukie na itoe mafuta.

 

MBOGA YA KISAMVU

 

Kisamvu fungu 1 kubwa

Nazi 3

Vitunguu ¼  kilo

Chumvi kiasi

1                    Kichambue kisamvu ukikatekate ukipike mpaka kilainike.

2                    Kuna nazi  uchuje tui zito zito. Kata vitunguu vyembamba vyembamba.

3                    Maji yakishakauka tia vitunguu utie na tui upike mpaka tui likauke. kisha epua.

 

MBOGA YA KABICHI

 

Kabichi kilo 1

Vitunguu ½ kilo

Samli ¼ kilo

Mayai 4

Tungule ¼  kilo

Pilipili manga kiasi

Chumvi kiasi

1                    Likate kate kabichi ulioshe ulpike mpaka liive.

2                    Kata vitunguu, katakata tungule na zisage pilipili manga.

3                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Tia tungule ukaange, tia kabichi, tia chumvi na pilipili manga. Kisha vunja mayai uyapige utie. Koroga mpaka likauke. kisha epua

 

MBOGA YA MAGANDA YA MAMUNG’UNYA

 

Maganda ya mamung’unya kiasi

Vitunguu ¼ kilo

Tungule ¼ kilo

Mayai 4

Samli kiasi

Chumvi kiasi

Pilipili manga kiasi

1                    Yakate kate maganda ya mamungunya madogo madogo kama vitunguu, uyapikekwa maji mpaka yaive.

2                    Kata vitunguu, ukatekate tungule na usage pilipili manga.

3                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Tia tungule ukaange, kisha yatie maganda pamoja na chumvi na pilipili manga. Vunja mayai uyapige uyatie. Koroga kidogo, ikikauka epua.

MCHUZI WA SAMAKI

 

Samaki kilo 1 (vizuri akiwa nguru)

Vitunguu maji ½ kilo

Nyanya ½ kilo

Vitunguu thomu kiasi

Samli ¼ kilo

Mbatata ½ kilo

Mdalasini kiasi

Pilipili mbichi kiasi

Bizari nzima kiasi

Hiliki kiasi

1        Mkate samaki umwoshe. Mtie chumvi na ndimu mkaange.

2        Kata vitunguu saga tungule, saga vitunguu thomu pamoja na viungo vyote vilivyobakia. Chemsha mbatata uzimenye.

3        Teleka sufuria utie samli. Ikichemka tia vitunguu maji uvikaange. Vikianza kupiga wekundu tia tungule. Kisha tia viungo vyote ulivyovisaga. Halafu tia mbatata na baadae utie vipande vyote vya samaki. Tia ndimu, chumvi na maji kidogo. Wacha vichemke kidogo. Onja ukiona kila kitu sawa, epua.

 

MCHUZI WA SAMAKI WA NAZI

 

Samaki kilo 1

Vitunguu ½ kilo

Tungule ¼ kilo

Nazi 2 au 3

Pilipili mbichi chembe 2 au 3

Limau kiasi

Chumvi kiasi

1        Mkate kate samaki, umuoshe. Mtie chumvi, ndimu na umsagie pilipili.

2        Saga vitunguu na tungule utie juuyake. Ukipenda pilipili mbichi unaweza kuzikatia pamoja na bizari. Tia vyote juu ya samaki. Mpike mpaka akauke maji yote.

3        Kuna nazi uchuje tui zito utie juu yake. Acha achemkie mpaka ashikane. Onja ukiona sawa epua. Usiache samaki akakauka sana, acha kidogo awe na rojo.

 

MCHUZI WA NYAMA

 

Nyama kilo 1

Mbatata kilo 1

Vitunguu ½ kilo

Tungule ½ kilo

Samli ¼ kilo

Limau kiasi

Chumvi kiasi

Bizari nzima kiasi

Hiliki kiasi

Mdalasini kiasi

Thomu kiasi

1        Kata nyama uipike kwa maji na chumvi mpaka iive.Epua na itizame, isiwe kavu bali iwe na supu.

2        Menya vitunguu uvikate, menya mbatata ukikate, saga tungule na thomu, saga vitu vyote vilivyobakia (yaani mdalasini, bizari na hiliki).

3        Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange na vikianza kupiga wekundu tia tungule, mbatata na viungo vyote vilivyobakia. Tia vipande vya nyama bila supu ukaange kidogokisha tia supu na ndimu uache ichemke kidogo. Onja chumvi ukiona kila kitu sawa epua.

 

MCHUZI WA NYAMA NA DENGU

 

Nyama kilo 1

Dengu ¼ kilo

Vitunguu ½ kilo

Tungule ½ kilo

Samli ¼ kilo

Thomu kiasi

Zabibu nyeusi kiasi

Bizari nzima kiasi

Hiliki kiasi

Mdalasini kiasi

Limau kiasi

Chumvi kiasi

1                    Kata nyama, osha dengu, tia maji na chumvi upike pamoja mpaka viive.

2                    Kata vitunguu, menya thomu usage. saga tungule na viungo vilivyobakia.

3                    Teleka sufuria utie samli. ikichemka tia vitunguu uvikange mpaka vipige wekundu. Tia tungule ukaange pamoja na viungo vyote vilivyobakia. Tia zabibu pamoja na nyama na dengu. Tia maji kidogo, limao na chumvi. acha ichemke kidogo. Ukiona kila kitu sawa epua.

 

MCHUZI WA NYAMA NA MCHICHA

 

Nyama kilo 1

Mchicha mafungu matatu

Vitunguu  ¼  kilo

Tungule ½ kilo

Samli ¼ kilo

Ukwaju kiasi

chumvi kiasi

1                    Teleka nyama uipike kwa maji na chumvi.

2                    Chambua mchicha, kata vitunguu pamoja na tungule.Roweka ukwaju uukamue.

3                    Teleka sufuria utie samli. Ikichemka tia vitunguu uvikaange, tia mchicha uukaange, tia tungule ukaangie pamoja. Tia nyama na supu yake yote na mwishowe utie ukwaju. Onja chumvi, ukiona kila kitu sawa epua.

 

MCHUZI WA KABABU

 

Nyama iliyosagwa kilo 1

Vitunguu ½ kilo

Mbatata ½ kilo

Samli ¼ kilo

Tungule ¼ kilo

Bizari nzima kiasi

Tangawizi mbichi kiasi

Mdalasini kiasi

Hiliki kiasi

Majani ya kotmiri fungu 1

Karafuu chembe 2 au 3

Limau kiasi

Chumvi kiasi

1                    Ioshe nyama uiweke katika kumto la nazi ivuje maji yote.

2                    Kata vitunguu, saga tungule, menya thomu usage, saga na viungo vyote vilivyobakia,ila majani ya kotmiri yaoshe uyachambue.

3                    Chukua nyama pamoja na nusu ya viungo ulivyovisaga uchanganye. Tia chumvi pamoja na limau ufinyange madonge madonge kama kababu. Teleka sufuria juu ya moto utie maji kiasi, chukua zile ‘kababu’ uzitie ndani ya maji (lakini hakikisha maji yamechemka.) Acha kababu zichemke mpaka zishikane barabara halafu ziepue uyachuje maji yote. ziache katika chujio lakini maji usiyamwage.

4                    Teleka sufuria utie samli. Ikichemka tia vitunguu uvikaange. Vikianza kuwa vyekundu tia tungule kisha tia viungo vyote, pamija na kotmiri. Kata mbatata nyembamba uzitie ukaangie pamoja. Tia kababu, tia chumvi pamoja na limau. Acha ichemke, mbatata ziwive. Ukiona kila kitu sawa epua.

 

MCHUZI WA KIMA (NYAMA YA N’GOMBE YA KUSAGA)

 

Nyama iliyosagwa kilo 1

Vitunguu ½ kilo

Tungule ½ kilo

Mbatata ½ kilo

Samli ¼ kilo

Thomu kiasi

Bizari nzima kiasi

Hiliki kiasi

Mdalasini kiasi

Chumvi kiasi

Tangawizi mbichi kiasi

1                    Osha nyama utie katika chujio au kumto ivuje maji.

2                    Kata vitunguu, tungule, menya mbatata uzikate nyembamba. menya thomu usage, saga na viungo vyote vilivyobakia.

3                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu ukaange. Vikianza kupiga wekundu tia tungule na mbatata. Kaanga kidogo. Baadae tia viungo vyote pamoja na nyama. Kaanga kidogo na utie maji pamoja na limau na chumvi. Acha ichemke mpaka karibu na kukauka. Onja, ukiona sawa epua.

 

MCHUZI WA MAINI

 

Maini kilo 1

Vitunguu ½ kilo

Tungule ½ kilo

Samli ¼ kilo

Thomu kiasi

Bizari nzima kiasi

Pilipili manga kiasi

Hiliki kiasi

Chumvi kiasi

Tangawizi mbichi kiasi

1                      Yakate maini uyaoshe. Menya vitunguu uvisage. Menya tungule uzisage. Menya tomu usage pamoja na viungo vyote vilivyobakia.

2                      Yachanganye maini pamoja na vitu vyote hivyo utie na chumvi na samli, uyateleke. Pika mpaka yakauke maji yote libaki rojo rojo na samli. Onja, ukiona kila kitu sawa epua.

MCHUZI WA UBONGO

 

Ubongo kilo 1

Vitunguu ½ kilo

Tungule ½ kilo

Samli ¼ kilo

Thomu kiasi

Bizari nzima kiasi

Hiliki kiasi

Pilipili manga kiasi

Mdalasini kiasi

Chumvi kiasi

Tangawizi mbichi kiasi

Limau kidogo (ukipenda)

1                    Uoshe ubongo upachuepachue uweke katika chujio uvuje maji.

2                    Kata vitunguu, saga thomu, tungule pamoja na viungo vyote vilivyobakia.

3                    Teleka sufuria utie samli.Ikichemka tia vitunguu uvikaange mpaka vipige wekundu. Tia tungule ukaange. Kisha tia viungo vyote ulivyovisaga. Mwisho tia ubongo ukaange. Baadae tia chumvi, limau na maji kidogo. Acha uchemke, ukikauka epua.

 

MCHUZI WA KUKU

 

Kuku mkubwa 1

Vitunguu ½ kilo

Tungule ½ kilo

Samli ½ kilo

Mbatata ½ kilo

Thomu kiasi

Bizari nzima kiasi

Hiliki kiasi

Chumvi kiasi

Limau kiasi

Karafuu chembe 2 au 3

1                    Mkate kuku umchemshe kwa chumvi na limau mpaka awive. Kata vitunguu.

2                    Teleka sufuria utie samli. Ikipata moto tia vitunguu ukaange. Kata vitunguu thomu usage. Kata tungule pamoja na viungo vyote vilivyobakia na ukaange pamoja. Tia mbatata na vipande vya nyama pamoja na supu yake. Acha ichemkekidogo kiasi cha kuiva mbatata. Angalia kama bado ina mchuzi yaani isiwe kavu. Onja, kama kila kitu ni sawa epua.

 

MCHUZI WA CHOOKO

 

Chooko ½ kilo (Adesi)

Vitunguu ¼ kilo

Tungule ¼  kilo

Samli  kidogo

Thomu kiasi

Hiliki kiasi

Nazi 2

Limau kiasi

Chumvi kiasi

1                    Osha chooko uzitie maji uziteleke. Acha zichemke mpaka ziive kisha epua.

2                    Kata vitunguu na tungule, menya thomu usage, saga na viungo vyote vilivyobakia. Kuna nazi uchuje tui zito.

3                    Teleka sufuria utie samli. Ikichemka tia vitunguu uvikaange. kisha tia tungule ukaange. Kisha tia viungo vilivyobakia. Baadae tia chooko pamoja na tui na limau kidogo. Acha zichemke na huku unakoroga. Onja chumvi, ukiona sawa epua.

 MAPISHI YA MWAMBAO MIKATE

HHHHHHHH

MKATE WA KUMIMINA

 

Mchele kilo 1

Nazi 3

Sukari ¼ kilo

Hiliki kiasi

Hamira kiasi (Inategemea hamira utakayoitumia)

1                    Twanga mchele uwe unga laini. kuna nazi uchuje tui zito. Twanga hiliki iwe  laini.

2                    Changanya unga, tui, sukari na hiliki ufinyange donge.litumbukize donge hilo ndani ya kinu kisafi. liponde mpaka lilainike. Litoe uliweke katika bakuli na utie hamira na tui. koroga mpaka uwe mchanganyiko mwepesi kidogo, uache uumuke.

3                    Washa moto itakuwa vizuri iwapo utatumia vifuu, vikishakuwaw makaaya moto, chukua tui kidogo ulisambaze kwenye sufuria yote. Iweke sufuria kwenye moto kwa muda mfupi. Ukiona tui linatoa mafuta iipue sufuria na umimine mchanganyiko ulioumuka. (Usitumie upawa kuchotea. Umimine tu wote mara moja.)

4                    Irudishe sufuria motoni (kwenye makaa) uifunike. Palia nusu ya makaa juu ya sufuria. Uache mkate uive, ukiwa unauangalia. Angalia ukiona unaanza kuwa mwekundu, chukua kijiti uuchome mpaka ndani. Utakapokitoa na kukiona kikavu, jua kuwa mkate umeiva. Uepue uache upoe.

 

MKATE WA CHILA

 

Mchele kilo 1

Sukari ¼ kilo

Nazi 3

Hiliki kiasi

Hamira kiasi (Inategemea hamira utakayoitumia)

Samli kidogo

1        Twanga mchele uwe unga laini. Kuna nazi uchuje na kutenga tui zito mbali na tui jepesi mbali. Twanga hiliki iwe laini.

2        Changanya unga wa mchele, sukari hiliki na hamira, kisha ufinyange donge kwa maji ya nazi. Chukua hilo donge la unga ulitie katika kinu kilichooshwa vizuri uliponde mpaka lishikane na lilainike barabara. Litoe ulitie katika bakuli na ulivuruge kwa kutia tui zito. Tia tui zito na huku unakoroga kwa upawa mpaka uuone unga umekuwa mwepesi kama uji, ila usiwe mwepesi sana tui lililobakia liweke.

3        Chukua tui lililobakia ulichanganye na sukari kidogo na hiliki ulipike na huku unalikoroga mpaka liwe zito zito, kisha liepue uliweke.

4        Unga ukishaumuka, teleka chuma, uchukue samli kidogo kwa kumbi la nazi usugulie juu ya chuma. Halafu teka unga kwa upawa  uutie juu ya chuma , ila usiutandaze uache utawanyike wenyewe . Chukua mkungu ulio safi  ufunike. Baada ya muda mfupi funua uutazame, ukiona umeshakauka utoe mkate uuweke kwenye sahani .

5        Chota kwa kijiko lile tui ulilolipika upakaze juu ua mkate. Endelea kuchoma kikate mpaka umalize unga wote.

 

MKATE WA UFUTA

 

Unga wa ngano kilo 1

Nazi 1 

Samli ¼ kilo

Ufuta kiasi (usafishwe vizuri)

      Hamira kiasi  (inategemea hamira utakayoitumia)

      Chumvi kiasi

1                    Kuna nazi uchuje tui zito.

2                    Chunga unga uvuruge kwenye tui, hamira na chumvi mpaka ulainike. Usiwe mzito sana wala mwepesi sana .Kisha uache uumuke.

3                    Unga ukishaumuka, washa moto wa makaa uteleke chuma kilichooshwa vizuri. Kikishapata moto kinyunyuzie maji. Kata donge la unga uliweke kwenye chuma. Litandaze kwa vidole mpaka liwe duara. Chukua ufuta kidogo kwa vidole unyunyuzie kwenye unga.

4                    Baada ya muda mfupi geuza chuma ili uso wa mkate upate moto. Mkate ukibadilika rangi na kuwa mwekundu ubandue kwa kutumia kisu uweke kwenye sahani unyunyuzie samli iliyoyeyushwa. Hapo mkate wa ufuta uko tayari kwa kuliwa.

5                    Endelea kuchoma mikate mengine mpaka unga wote umalizike.

 

MKATE WA MAYAI

 

Mayai 6

Sukari kiasi cha vikombe vitatu vya kahawa

Unga wa ngano kiasi cha vikombe vitatu vya kahawa

Hiliki kiasi

Samli kidogo

Zabibu kiasi

Arki kidogo

Baking powder nusu kijiko cha chai

1                    Changanya unga mkavu na Baking Powder.

2                    Chukua bakuli lenye nafasi utie sukari. Menya hiliki uzitwange. Kisha zichanganye na sukari na utie arki uipendayo. Vunja mayai yote utie. Chukua mchapo wa kupigia mayai uyapige mpaka yajae kiasi cha kutosha.

3                    Chukua unga uwe unautia na huku unakoroga mpaka umalizike wote.

4                    Chukua sufuria uipake samli iliyoganda pembezoni mote. Kisha mimina mayai yote ufunike. Upike mkate kwa moto wa mkaa, juu na chini. Angalia moto usiwe mkali sana. Utaunguza mkate. Moto uwe wa kiasi. Mkate ukianza kupiga wekundu chukua kujiti uuchome mpaka ndani. Ukiona kimetoka kikavu jua kuwa mkate umeshaiva. Uepue uache upoe. Baadae utoe kwa upole uweke kwenye sahani. Chukua zabibu tia ndani ya maji ya moto kidogo zipate kuregea. Baadae zipage juu ya mkate ukishaanza kupiga wekundu ndio uzitie.

 

MKATE WA KUKAANGA KWA MAZIWA NA MAYAI

 

Maziwa ½ painti

Samli ¼ kilo

Mayai 3

Chumvi kiasi

Pilipili manga kiasi

Boflo 1 kubwa

1        Kata mkate wa boflo vipande vya kiasi. Piga mayai pamoja na chumvi kidogo na pilipili manga.

2        Teleka chuma utie samli. Ikianza kuchemka chukua vipande vya mkate uvichovye katika maziwa na baadae  uvichovye katika mayai kisha uvitie katika chuma uvikaange. Vikiwa vimewiva upande mmoja geuza upande wa pili. Vikiwa tayari vitoe uvitie kwenye sahani.

 

MKATE WA MAYAI NA JAM

 

Boflo kubwa 1

Mayai 4

Unga wa ngano kidogo

Jam kidogo

Samli ¼ kilo

1        Kata mkate vipande vyembamba vyembamba  uvipake jam, kisha vigandanishe kimoja juu ya kingine.

2        Vunja mayai uyapige sana. kisha nyunyizia unga huku ukiendelea kuyapiga mayai.

3        Teleka chuma utie samli. Ikianza kuchemka vichovye vile vipande vya mkate ndani ya mayai na uvichome ndani ya samli. Vikiiva upande mmoja geuza upande wa pili kisha uvitoe uvitie kwenye sahani.

 

MKATE WA KINGAZIJA

 

Unga wa mchele kilo 1

Sukari ¼ kilo

Nazi 4 kubwa

Mdalasini  gram 100

Bizari nzima kiasi

Hiliki kiasi

1        Kaanga sukari mpaka iwe nyekundu. Kuna nazi zote uchuje tui zito zito. Ligawe tui sehemu mbili. Litie sehemu moja katika sukari uliyoikaanga ulipike na huku unalikoroga mpaka iyeyuke sukari yote. Liepue uliwache lipoe.

2        Twanga bizari, mdalasini na hiliki. Uchunge unga wa vitu hivyo kisha uchanganye na  unga wa mchele. Baadae uchanganye na hilo tui lililopikwa. Ukoroge unga mzito mzito.

3        Chukua tui bubu ulilolibakisha ulipike kando mpaka litoe mafuta na baadae uligawe sehemu mbili. Sehemu moja lipakae katika sufuria na sehemu nyengine uliweke.

4        Mimina unga katika ile sufuria uliyoipaka tui kisha utafute sufuria nyengine iliyo kubwa zaidi utie maji na utumbukize ile yenye unga ndani yake upike kama unavyopika “Pudding”. Kila yakikauka maji tia mengine na utapotia ukoroge ule unga na uusonge mpaka uive. Ukisha iva uweke sawa kwa mwiko na uchukue lile tui ulilolibakiza ulitie juu ya mkate na pembezoni mote na kisha upalie moto. Angalia, ukiona umeshakuwa mwekundu na umeiva vizuri utoe kwa upole utie kwenye sahani upoe.

 

MKATE WA MANDA

 

Unga wa mchele kilo 1

Nazi 3 kavu

Chumvi kiasi

Kitunguu maji ¼ kilo

1        Kuna nazi usiichuje. Kata vitunguu vyembamba. Changanya unga na nazi pamoja na vitunguu ukande vyote pamoja kwa maji ya chumvi. Kanda mpaka unga ushikane uweze kukatika madonge madonge.

2        Chukua majani ya mgomba uyakatekate kisha yaweke katika gae au kikaango kilicho kipana chenye nafasi. Baadae ukate unga madonge madonge uyaweke juu ya majani ya mgomba. Funika majani mengine juu ya mikate (Yaani weka jani moja chini ya unga na jani moja juu yake) Baadae ufunike kwa mkungu uchome kwa moto juu na chini. Angalia, ukiona mikate imeshaiva kwa kupiga wekunduitoe utie kwenye sahani.

 

MKATE WA AJEMI

 

Unga wa ngano kilo 1

Samli kidogo

Hamira kiasi  (inategemea hamira utakayoitumia)

Soda kidogo

Chumvi kiasi

1        Changanya unga, samli kidogo sana,  soda, hamira na chumvi, na ukande kwa maji, usiwe mgumu wala laini sana. Kisha uache uumuke.

2        Uchukue unga baada ya kwisha umuka ukate madonge madonge.

3        Weka chuma juu ya moto mdogo wa mkaa. Kisha ulichukue donge moja ulisukume na uliweke kwa upole juu ya chuma. Ukiwa unahisi kuna unga unaweza kuganda juu ya chuma chako, unaweza kupaka samli kidogo juu yake. Ufunike kwa mkungu uuchome kwa moto juu na chini. Baada ya muda mfupi uangalie, ukiona umeshatutumka na umekuwa wa rangi ya manjano utoe uchome mwengine. Endelea hivi hivi mpaka umalize mikate yote.

 

 

 

MKATE WA AJEMI WA KUKU

 

Kuku mkubwa 1

Samli kilo 1

UNGA ½ KILO

Vitunguu ½ kilo

Mayai 8

Limau kiasi

Thomu kiasi

Hiliki kiasi

Bizari nzima kiasi

Chumvi kiasi

Zaafarani kiasi

Baking powder kiasi

1        Mkate kuku vipande vipande umchemshe kwa maji, limau chumvi na bizari  mpaka akauke maji yote na aive.

2        Teleka sufuria umkaange kuku mpaka aive awe mwekundu kisha umtoe. Tia vitunguu uvikaange mpaka viwe vyekundu. Saga thomu, hiliki na bizari nzima utie. Roweka  zaafarani utie maji yake. Itoe nyama ya kuku mifupa bila ya kuivuruga halafu itie.

3        Fikicha unga na samli halafu utie maji ya moto uukande mpaka uwe laini, (na itakuwa vizuri ukitia ‘Bakingpowder.’) Ukate unga madonge mawili uyasukume kiasi ya legeni ulilonalo. Lipake legeni lote samli baadae utie ule unga uliosukuma sehemu moja. Vunja mayai manne juu ya unga, kisha tia vitu vyote. Tia mayai yaliyobakia yote bila ya kuyapiga. Halafu utie sehemu ya pili unga uliosukuma umfunike kuku wote na ushikanishe unga wa juu na chini kwa kuusokota sokota pembeni kote. Mimina samli iliyochemshwa juu yake kwa kunyunyuzia kila upande na baadae uchemshe kwa kutia moto mdogo juu na chini mpaka uive kuwa mwekundu bila ya kuungua.

4        Ukisha iva ukapoa, utoe utie kwenye sahani kwa utaratibu bila ya kuuharibu.

 

MKATE WA KUSUKUMA

 

Unga wa ngano kilo 1

Samli ½ kilo

Nazi 1

Chumvi kiasi

1        Kuna nazi uchuje tui zito. Chunga unga uukande kwa nazi na utie chumvi, ukande mpaka ulainike. Ukate unga madonge madonge kiasi cha mikate uitakayo, yaani ukitaka mikate mikubwa utakata madonge makubwa makubwa na ukitaka mikate midogo midogo, utakata madonge madogo.

2        Chukua kibao na kifimbo cha kusukumia unga, utie unga mkavu juu ya kibao uchukue donge moja uanze kusukuma. Sukuma hadi uwe duara, halafu uchukue samli iliyoganda upake mkate wote halafu uukunje namna yoyote upendayo, ikiwa unataka mkate uwe na ncha nne ukunje ukae ncha nne, ikiwa unataka duara usokote ukae duara. Endelea hivyo hivyo mpaka mikate yote imalizike.

3        Washa moto uteleke chuma. Kikipata moto tia samli uchukue donge la unga ambalo umeshalikunja ulisukume kwa kifimbo cha kusukumia na kuuweka juu ya chuma. Uchome kwa kuuzungusha zungusha ili upate kuiva pande zote. Ugeuze upande wa pili na uchome hivyo hivyo hadi uive. Endelea kuchoma mikate yote hivyo hivyo mpaka imalizike.

 

MKATE WA TAMBI

 

Tambi kilo 1

Sukari ¼ kilo

Nazi kavu 2

Hiliki kiasi

Arki kiasi

Zabibu kiasi

1        Teleka sufuria utie maji. yakichemka zitie tambi uache zichemke. Baadae zimimine katika kumto au chujio ili maji yote yagidike.

2        Kuna nazi uchuje tui zito. Menya hiliki uzitwange utie juu ya tui.

3        Teleka tui katika moto ulipike na huku uwe unalikoroga mpaka libaki kiasi cha tambi. Tia sukari pamoja na tambi na arki upike mpaka tui lote likauke.

4        Chukua legeni ulipake tui kidogo. Liweke juu ya moto li tui litoe mafuta halafu zimimine tambi zote ndani ya legeni uzilaze laze vizuri zikae kama mkate. Baadae chukua zabibu uzipambe vizuri juu ya mkate kisha ufunike mkungu utie moto mdogo juu na chini. baada ya muda ipua uwache upoe kidogo. Kisha utoe mkate kwa upole bila ya kuuharibu. Utaweza kuukata vipande vipande ukipenda.

 

MKATE WA CHANDARUA

 

Unga ¼ kilo

Samli ¼ kilo

Chumvi kiasi

1        Koroga unga uwe mwepesi, kuliko mkate wa maji, na utie chumvi.

2        Teleka chuma ukipakae samli kwa kutumia kumbi. Chovya vidole vyako katika unga umichie michie juu ya chuma na pembeni kote. Acha ukauke kisha uutoe kwa kisu taratibu bila ya kuugeuza. Unapoutoa utaona uwaziwazi kama chandarua.

 

MKATE WA NYAMA (MSANIF)

 

Unga kilo 1

Nyama ¾ kilo

Vitunguu kilo 1

Samli ¾ kilo

Nazi nzuri 1

Thomu kiasi

Tangawizi mbichi kiasi

Pilipili manga kiasi

Limau kiasi

Chumvi kiasi

Hamira kiasi (inategemea hamira utakayoitumia)

1        Saga nyama uikoshe. Kata vitunguu vodogo vidogo kama vya sambusa. Menya thomu uitwange pamoja na tangawizi mbichi na pilipilimanga. Changanya nyama na vitunguu pamoja na viungo ulivyovitwanga utie chumvi na ukamulie limau, kisha uipike mpaka ikauke maji iwe kavu, halafu iipue uitandaze ipoe.

2        Kuna nazi uchuje tui zito. Chunga unga uvuruge kwa tui na chumvi na hamira halafu uweke uache uumuke. Unga usiwe mzito sana.

3        Teleka chuma utie samli kisha chota unga kwa vidole vyako utie juu ya chuma utandaze duara kiasi cha kitumbua, halafu chukua kijiko uteke nyama uitie juu ya ule unga uenee mote. Teka tena unga mwengine ufunike ile nyama yote kisha kisha uchukue kisu uusogeze katikati ya chuma ili uive vizuri. Uache uchemkie juu ya samli na huku ukiugeuzageuza upate kuiva vizuri. Pindua upande wa pili uuchome kama mwanzo mpaka uive. Unaweza kuchoma mikate miwili au mitatu kwa wakati mmoja. Choma mikate yote mpaka unga na nyama imalizike.

 

VIKATE VYA ZAAFARANI

 

Mchele kilo1

Unga wa ngano ½ kilo

Samli ½ kilo

Sukari ½ kilo

Maziwa painti 1

Mayai 6

Hamira kiasi

Zaafarani kidogo (iroweke kwa maji ya moto robo ya kikombe cha kahawa)

1        Twanga mchele uuchunge unga laini. Twanga hiliki, changanya unga wa mchele na wa ngano, sukari na hiliki na arki. Tia samli iliyoyeyushwa ufikiche, tia hamira na maji ya zafaarani na uvunje yai moja moja na huku unaukanda mpaka yamalizike mayai yote. Kisha tia maziwa uchanganye mpaka uwe mwepesi kiasi. Inatakiwa uwe mzito kidogo kuliko wa vitumbua.

2        Teleka kijungu kidogo rashia samli kwa kutumia kumbi la nazi, kisha teka unga utie na ufunike. Wacha uive kwa muda mdogo, kisha geuza bila ya kutia samli nyengine. Baadae urejeshe upande wa mwanzo, ukiona umeshakuwa na rangi nyekundu ya kupendeza utoe. Inabidi uichome mikate hii kwa moto mdogo sana.

 

VIKATE VYA JOYA

 

Mchele kilo1

Sukari ¼ kilo

Nazi 3

Hiliki kiasi

Hamira kiasi (inategemea hamira utakayoitumia)

Zaafarani kidogo (iroweke kwa maji ya moto robo ya kikombe cha kahawa)

1                    Twanga mchele uchunge unga uwe lai i sana. Kuna nazi uchuje tui zito mbali na jepesi mbali.

2                    Changanya unga na sukari uufinyange donge kwa tui jepesi.

3                    Kosha kinu kiwe safi sana, utie hilo donge na uliponde kama unavyoponda unga wa mkate wa kumimina. Utoe ulitie katika chombo utie tui, hamira, hiliki na ukoroge uwe mwepesi sana. Uache uumuke.

4                    Teleka maji katika sufuria kubwa halafu uweke kitu chenye tundu tundu mfano wa waya. Chukua vibakuli vidogo vidogo vilivyopakwa tui umimine unga ndani yake uvipange vibakuli hivyo juu ya ule waya wenye matundu, na ufunike kwa mkungu. Acha maji yachemke kwa muda si chini ya dakika ishirini. Baadae angalia, ukiona vimeshaiva vitoe uvitie kwenye sahani utie dola la zafaarani juu ya vikate.

 

VITUMBUA

 

Mchele kilo 1

Sukari ¼ kilo

Nazi kubwa 2

Hiliki kiasi

Hamira kiasi (inategemea hamira utakayoitumia)

Samli au mafuta ½ kilo

Mayai 4 (ukipenda)

1        Uroweke mchele uutwange uwe unga laini. Kuna nazi uchuje tui zito. Menya hiliki uitwange.

2        Changanya na sukari na hiliki, tia hamira na utie tui uvuruge uwe na wepesi wa kuweza kutekeka kwa upawa, halafu uache uumuke.

3        Teleka vijungu vidogo, ikiwa kimoja viwili au zaidi, kadri uwezavyo. Tia samli katika hivyo vijungu, ikichemka teka unga kwa upawa utie katika hivyo vijungu na baadae uufunike. Uache kwa muda kidogo viive halafu geuza upande wa pili kwa kutumia kijiti kilichotengenezwa vizuri ukiona upande wa pili umeshaiva vitoe. Endelea kuchoma hivi hivi mpaka wote umalizike. (Kila wakati mafuta au samli ikipingua unaongeza).

 

VILOSA

 

Unga wa mchele kilo1

Sukari ¾ kilo

Samli kilo 1

Mtindi painti 1

Nazi  2 nzuri

Arki kiasi

Hiliki kiasi

Hamira kiasi

1                    Kuna nazi uchuje tui zito. Menya hiliki uzitwange.

2                    Changanya unga na sukari kidogo, hamira na mtindi, halafu uvuruge kwa tui hadi uwe mwepesi kuliko unga wa vitumbua. Uweke uumuke.

3                    Tia maji kidogo katika sufuria utie na sukari, hiliki na arki upike shira nyepesi ya kiasi.

4                    Unga ukishaumuka teleka vijungu kama vile vya kupika vitumbua utie samli. Ikichemka teka unga kwa upawa uanze kuvichoma vilosa. Tia unga katika vijungu kisha uvifunike. Wacha vitokote kwa muda mdogo kisha vitoe uviweke katika chujio vivuje mafuta, kisha vitumbukize katika shira. Endelea kuchoma mpaka vimalizike vyote.

 

MAANDAZI

 

Unga kilo 1

Sukari ¼ kilo

Samli kilo 1

Nazi 1

Hamira kiasi

Hiliki kiasi

Arki kiasi

1        Kuna nazi uchuje tui zito.

2        Changanya unga, sukari, hiliki, arki na samli kidogo ukande kwa tui la nazi mpaka ulainike kisha uache uumuke.

3        Kata unga madonge ya kiasi usukume na ukate kwa namna upendayo.

4        Teleka karai juu ya moto utie samli. Ikichemka tia vipande vya unga uchome maandazi, yakiiva upande mmoja geuza upande wa pili. Endelea kuchoma mpaka umalize unga wote.

 

 

MAANDAZI YA KIPEMBA

 

Unga kilo 1

Sukari ¼ kilo

Samli kidogo

Nazi 8

Hamira kiasi

Hiliki kiasi

Arki kiasi

Mayai 3

1          Kuna nazi uchuje tui zito. Menya hiliki uitwange.

2          Changanya unga, sukari, hiliki, arki, samli mayai na hamira ukande kwa tui la nazi mpaka uwe laini sana. Ukate unga madonge madonge halafu uusokote.Tafuta legeni lenye nafasi ulipakae samli. Uchukue ule unga uliokwisha sokota uuweke juu ya hilo legeni kwa nakshi uipendayo. Unaweza kufanya maandazi yenye nashi za aina mbali mbali. kisha uache uumuke.

3          Unga ukishaumuka usiutoe. Chukua sinia nyengine ufunikie juu yake na uyachome maandazi kwa kutia moto mdogo juu na chini.

4          Angalia, ukiona maandazi yameshaiva kwa kupiga wekundu yatoe uyaweke kwenye sahani.

 

KAIMATI

 

Unga ¼ kilo

Samli ½ kilo

Sukari ½ kilo

Yai 1

Arki kiasi

Hamira kiasi

Hiliki kiasi

1        Changanya unga, samli kidogo, yai na hamira uvuruge kwa maji, usiwe mwepesi wala mzito sana. Uweke upate kuumuka.

2        Chukua hiliki uzimenye na kuzitwanga.

3        Teleka sufuria utie maji sukari, arki na hiliki uache ichemke mpaka iwe shira nyepesi.

4        Teleka karai utie samli. Ikianza kuchemka anza kuchoma kwa kuchota unga kwa vidole utie katika karai. Choma kaimati ndogo ndogo zenye umbo kama ndimu. Zichome kwa kuzigeuza geuza katika mafuta mpaka ziwe na rangi ya manjano. Zitoe uzitie katika chujio zivuje mafuta, kisha zitumbukize katika shira zipate kuingia shira ndani. Baadae zitoe uziweke kwenye sahani.

 

MKATE WA NYAMA (MTABAK)

 

Nyama ½ kilo

Vitunguu maji ½ kilo

Samli ½ kilo

Unga ¼ kilo mayai 4

Pilipili manga kiasi

Bizari nzima kiasi

Tangawizi mbichi kiasi

Vitunguu thomu kiasi

Baking Powder ½ kijiko cha chai

Limao kiasi

Chumvi kiasi

1        Osha nyama iliyokwisha sagwa uichuje maji yote. Menya vitunguu uvioshe uvikate vidogo vidogo kama vya sambusa. Menya vitunguu thomu usage pamoja na tangawizi mbichi. Twanga pilipilimanga pamoja na bizari nzima.

2        Changanya nyama na vitunguu pamoja na viungo vyote ulivyovisaga na kuvitwanga, tia chumvi na limau. Ipike nyama pamoja na viungo vyote mpaka ikauke. Epua uitandaze ipoe.

3        Chunga unga uufikiche kwa samli iliyoyeyushwa utie Baking Powder uukande kwa maji yaliyotiwa chumvi kidogo mpaka ulainike. Ukate unga madonge mawili. Tia unga mkavu juu ya kibao cha kusukumia, usukume uenee kibao chote. Vunja yai moja ulitie katikati ya unga uliousukuma ulitandaze. Chukua nyama utie juu ya lile yai na uitandaze ikae pembe nne, kiasi cha inchi 6 kila upande. Vunja yai la pili juu ya nyama na baadae ufunike kwa ule unga uliobakia pembeni kama bahasha ya pembe nne. Fanya mkate wa pili kwa vitu vilivyobakia kama wa kwanza. (Kwa sababu vipimo tulivyotoa ni vya mikate miwili).

4        Teleka chuma juu ya moto utie samli. Ikipata moto tia mkate uuchome kwa utaratibu, hautaki moto mkali ukishaiva upande wa kwanza geuza upande wa pili na ukiiva utoe uchome wa pili hivyo hivyo.

 

 

 

 

Advertisements

152 Replies to “MAPISHI”

  1. Waaleykum salaam, Bi Asha ahsante sana namshukuru Allah kwa kujaalia Blog hii kuwanufaisha watu kwa ajili yake. Nami nawatakia kila la kheri wote wanaotembelea Blog hii. Allah atawalipa kila la kheri INSHAALLAH.

   1. assalamu alaikum nimesomea upishi nashukuru hii blog imenisaidia kujua vitu vingi mwenyezi mungu awajalie inshallah

   1. Asalaam aleykum! Ahsante kwa kutembelea Blog ya Mwanamke wa Kiislam. Kuhusu suala lako ndio tungule ni nyanya za majani au nyanya za maganda.

  1. Asalam aleykum,
   Ahsante sana kwa suala lako tungule ni nyanya au tomato.
   Ahsante endelea kufaidika na Blog ya Mwanamke wa Kiislam.

 1. Assalam Aleykum,

  Nimefurahishwa na mapishi mazuri mno na kama yapo zaidi naomba unitumie kwenye email yangu.

  SHUKRAN

 2. sio siri binafsi na kama mwanamke ninaipenda sana safu ya mapishi kwani mwanamke mapishi eeeeeeeeeee! kwahivyo aksanteni kwa elimu hiyo adhimu. ila tafadhali niambie maana ya maneno zaafarani,mbatata,majani ya kotmiri na majani ya nanaa na je, kama siwezi tumia samli nitumie mafuta gani badala yake? pia naomba kama itawezekana mnitumie mambo haya kwenye email address yangu.

 3. mapishi mazuri sana(very delicious} ila naomba ingependeza na kuuvutia zaidi mngeeka na picha kwa chakula husika,mfano wali wa asumini muweke ile picha yake-naamini itavutia saaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaana.pia naomba mnitumie kwenya email yangu.nangeshauri muweke na vipodozi vya asili maana siku hizi wanawake wingi wanajiumbua kwa makemikali na kujiharibu sura zao evenif wanataka uzuri lakini watumie njia mbadala sio makemikal.naomba kama itawezekana kwa moambi hayo.ahsante

 4. kwakweli mapishi yenu mazuri kweli yanaeleweka muko juu km mawingu me ni mpenzi mzuri wa mapish na nimevutiwa kweli na mapishi yenu hongereni sana ila muwe munaeka na picha itavutia zaidi

 5. Mapishi ni bomba sana ila nina swali unaposema vitunguu kilo moja mm sijaelewa naona kama ni vingi ni kilo moja au kimoja hapo sijakuelewa vizuri

  1. jamani sijaelewa tungule, nielewesheni jamani. na katika kupika mchuzi wa nyama sijaona matumizi ya hoho, karoti, na nyanya au vitu hivi havitakiwi kwenye mboga?. nisaidieni mie

   1. Ahsante kwa kutembelea blog ya Mwanamke wa Kiislam.
    Kuhusu suala lako tungule ni nyanya na vitu vyengine kama carrot unaweza kutumia katika mapishi ya mchuzi wa nyama.
    Endelea kufaidika na Mwanamke wa Kiislam.
    Ahsante sana.

 6. kwa kweli hhi blog ni nzuri lakini ni bora mngetumia maneno ambayo ni comfotable kwa baadhi ya watu ambao kiswahili chao ni tofauti na wengine na sio yale ya asili zaidi ahsante.

 7. A’alykum! Asanteni kwa mapishi m/mungu awajaalie kheri zaid ktk Mwezi huu wa ramadhan, naomba kufahamishwa kupika Vitumbua vya nyama,kuku au samaki.

 8. napenda sana mapishi yenu ya na wasaidia wengi wasio juwa bazi ya zitu vya kupika pia kuna majina ya viungo andikeni kwa luga watu wanayo ijuwa kwani siyi wote wanaojuwa thomu,arki.tungule

  1. Nashkuru kwa kuitembelea blog ya Mwanamke wa Kiislam ahsante.
   Kuhusu suala lako arki ni aina fulani ya marashi ambayo hutia harufu nzuri katika chakula zinakuwa kwenye vichupa maalum.

 9. Nimeipenda Blog yenu kwani sasa nimekamilika kuwa mwanamke haswaa! Hata mume wangu ameona tofauti ya chakula cha nyumbani na mama ntilie.

  Asalam Aleikum

 10. jamani,nadondosha mate huku nkisoma. Elimu ni wa kweli tena twashukuru huku Mombasa. Inshaallah Rabuka awazidishie mema hapa duniani na hata kesho mkienda akhera.

 11. AISE HIINI ZAIDI YA MAPISHI YOTE AMBAYO NINAYAJUA NAKUSEMA NI MATAMU MUNGU AKUBARIKISANA KWANI UMETUELIMISHA WENGI SIO KILASIKU ULE WALI,UGALI KUMBE KUNA VITU VYENGINE UNAWEZA UKAPIKA WATU WAKAJILAMBA

 12. A.alaykum,dah!namshkuru Mweyezimungu kwa kuwapa wazo na upeo wa kuuelimisha umma,ktk swala zima la mapishi….nimefunzika kwa elimu mnayotoa.Maashaallah,Mwenyezimungu awalipe heri inshaalla!

 13. assalam alaykum.
  jamani nimejifunza zaidi ya vile nilivyokuwa ninavijua,
  ninawasifu, kazi nzuri na allah awape kheri.
  ila jamani tungule ndio nini? na ninaomba mtuandikie maelekezo
  kwa kiswahili na kiingereza.
  pia ninasuggest muweke picha
  ya chakula pamoja na jina lake iwe rahisi
  kutambua output ya upishi.
  wabillahi tawfiq.

  1. Waaleykum salaam, Nashukuru sana kwa kuitembelea Blog hii Tungule ni tomato.
   Ahsante endelea kufaidika na Blog ya Mwanamke wa Kiislam.

 14. A,alaykum! nimefurahishwa na blog yenu ya mapishi, allah awazidishie….! naomba kama itawezekana mnitumie mapishi katka e.mail yangu.

 15. as.aleikum. Asante sana kwa blog hii nime penda sana mapishi yaliopo inshllhl allah atawa zidishia kila la khery……

 16. Assalam Aleykum
  Kwa kweli wamesema wote ila mapishi hayo ni mazuri sana na nimevutiwa nayo
  Keep it up na utufunze zaid na zaid. Pia uongeze na mengine pia
  Shukran

 17. as, alaykum warahmatullah wabarakatuh! asante kwa mapishi mazuri na yanahamasisha hata kama mtu hapendi kupika au hajui atajaribu ila nimetatizika sana na lugha iliyotumiwa kwa mfano mkungu na mengine tafadhali unapomaliza ni vizuri ukatafsiri baadhi ya maneno ili mpishi aelewe, na pia nimeona mahitaji ya vitu ni kipimo kikubwa sana. je asiye na uwezo mkubwa anatumia vipi vipimo hivyo? tafadhali nijibu kwa faida zaidi ya kazi kubwa uliyoifanya ili mpishi aweze kupatia kile ulichofundisha wengine hawajawahi hata kuuona huo mkate wa chandarua lakini wangependa kujaribu kupika, unaonekana ni rahisi na hauna gharama kwa hiyo picha ya vyakula unavyopika ni muhimu kuweka tazama mapishi alhidaya! tafadhali naomba majibu.

  1. Asalam aleykum, kuhusu mkungu ni ufuniko uliotengenezwa kwa udongo. Na kuhusu mahitaji mtu atakisia na kupika kiasi ya uwezo wake.
   Endelea kufaidika na Mwanamke wa Kiislam.

 18. ASSALAM ALAYKUM KWA KWELI NIMEVUTIWA SANA NA UKURASA HUU WA MAPISHI.JE MNAWEZA KUNITUMIA NAKALA KATIKA EMAIL YANGU.
  PILI JE NAWEZA KUPATA VIDEO INAYOHUSIANA NA KURASA HII.

  1. Waaleykum Salaam ahsante kwa kutembelea Blog ya Mwanamke wa Kiislam. Kuhusu kukutumia inawezekana lakini nasikitika hakuna video ya mapishi haya.
   Ahsane endelea kufaidika na Mwanamke wa Kiislam.

  1. Asalaam aleykum, arki ni essence au ni aina ya flavour ya kuongeza harufu na ladha katika chakula mfano kama rose, vanilla na nyenginezo. Natumai nimekujibu vizuri INSHAALLAH. Ahsante sana endele kufaidika na Blog ya Mwanamke wa Kiislam.

 19. Asalaam alaykum, nimefurahishwa sana na safu hii ya mapishi. umenigusa sana ukhut kwa napenda sn kupika Allah akuzidishie ujuzi mpate kutunufaisha,kwani hata ndoa sasa zitajaa furaha.

 20. shukran kwa kutuelimisha Allah awafanyie wepec.ushaur wangu ni juu ya vipimo munavotuwekea.bora vipimo viwe ni vidogo na kama mtu anataka kupika chakula kingi atakisia yy mwenyewe kwa kuongeza.

 21. Asalaam aleykhum.. mashallah mapishi yanatia raha.pia tuwekeeni vipimo kwa wale wanaishi wawili ukiangalia hayo ni mapishi ya familia kubwa na ukitamani kupika inaweza ikwa israfu …

  shukrani

 22. Assalam Alaykum, Ahsante sana nimependa sana mapishi yenu mazuri na hasa ukizingatia mimi ni mmoja wapo mwanamke wa kizanzibari ila nilikuwa nna ombi langu naomba tafadhali mutuwekee mambo ya urembo wa asili na jinsi ya kumtunza mume kwa njia zote.

  Ahsante.

 23. Hii ni moja ya Saiti nzuri sana, na Mwenyezi Mungu awazidishie na awape nguvu zaidi, na mimi unitumie kwenye email nataka kufungua hoteli hivyo nitakuwa nikiitumia

 24. beautiful really proud to be african.ni raha sana kuweza kuwa na wanawake walio na passion na chakula ,kwani haswa vyakula vya kwetu ni vizuri mno,mimi ni chef lakini vyakula vya nyumbani mmenisaidia sana nikurudi nyumbani napika vya nyumbani kwa confidence kabisa.Well done .Judith

 25. Jazakalaul kheir,kweli tumenufaika,kama mtu hataki kupika basi ni yeye mwenyewe.Kama si usumbufu naombeni mnitumie kwenye email yangu,Allah awajaze.

  1. asalaam aleykum warahmatullah wabarakatuh, nimefurahishwa na mapishi yaliyomo humu, naomba inshaallah yakiwepo zaid ya hayo mnitumie kwenye email yangu.

 26. nimefurahishwa kwa kutumia uasili wa vinu na majiko ya makaa na chakula kinakuwa kizuri si wote wenye blender na oven. ninaomba mutufundishe vitu kama icecream na michanganyiko ya juice. shukran sana.

 27. NIMEFURAHI SANA KWA KUTUPA MAELEKEZO YA MAPISHI ANGALAU FAMILIA ZETU ZIFURAHI KWA KUWABADILISHIA VYAKULA ALLAH AKUZIDISHIENI ZAID YA HAYA.

 28. Ahsanteni yani nimejifunza mengi nashkuru ambayo nilikua siyajui na nilokua nayajua nimepata kuongeza ujuzi mana kuna mambo mapya nimegain..thanx for being with us like this I realy enjoy my self..thanx alot

 29. Aslam aleikum, hongera sana kwa ukurasa huu Allah awazidishie hawape afya na uzima hili muendelea kutufuza namna ya kupika cookies na keki. INSHALLAH

 30. hongera sana kwa mapishi niko mbioni kupika karibu kila kitu cha hapa loh mwanamke mapishi!hivi inawezekana kupata updates za mapishi kwa email yangu?

 31. Asante sana kwa blog hii nzuri tunaomba kama una aina nyingi zaidi za mapishi uendelee kutuelimisha na myaazi mungu atakubariki inshaalah. Kama ujuavyo umeboresha mahusiano ya walio wengi, si unajua mwanamke jikoeeeeeeeeeeeeee!

 32. nimependa sana huu ukurasa wa mapish utanisaidia sana kwa mm ninae soma muda mwingi nipo chuoni nikirudi home nitakuwa napikaaa mapish mbali mbali napenda muwe munabadilisha mapish ya signe tofaut

 33. mashaallah mapishi mazur nimenufaika na mengi allah awazidishie iman na elimu zaid mzid kutuelimisha nac nilpenda munitumie mapishi mengine kwenye email yngu plzz

 34. jazaki llah kheir ukhty umetusaidiana sana mie ni mzanzbar nliondoka huko nkiwa mdgo cjajua kupka ila majina ya vyakula nayajua bas nataman lakin kupka cwez. nmepata kujifunza hapa na practice umetumia lugha nzur yenye kuelewek

 35. Nimependa sana mapishi yenu na mimi napenda sana kupika na kujifundisha. Siku zote zanzibar upo juu kwa mapishi.

 36. mashaallah mapishi mazuri ila naomba kujua maana ya lageni na naomba pia kama kuna mapishi mengine mapya naomba mnitumie kupitia email yangu hapo juu m/ mungu awazidishie

 37. Assalam aleykum hakika nimeipenda sana hii saafu ya mapishi mimi binafsi nikiwa mpenzi wakupika lakini huwapa mafunzo akina mama wenzangu nimepata mapishi mapya yakuzidi kuwaelimisha wenzangu. Mwenyezi Mungu atakulipa na hii ilmu iwe sadaqatul jaaliyah kwako na kwetu sote tutakao wafikishia wengine. Shukran jazilah.

 38. nimeipenda sana kurasa yenu. ila jaribun kutumia kiswahili rahisi zaidi wengine tunapata shida kidogo kuelewa haswa kwenye mahitaji.

 39. Wow thanks for ur teaching mumenisaidia sana jazakaallah kher allah awazidishie na ningewaomba pia munikumbuke kwa kunitumia mapishi zaid tafadhalini

 40. vyakula ni vitamu ,ombi langu ni kwamba majina ya mahitaji yaandikwe kwa lugha mbili yaani Kiswahili na kiingereza .Mungu akubariki sana.

 41. Asalaam.aleykum nmenufaika na mengi sana katika hili aswa naend olewa hv karbuni asnte sanaa kwa mapishi yako dada asnt sanaa ubarikiwe wabbilah tawfiq

 42. Nmependa sana na hongera kwa kutuletea hii, ila kidogo Lugha inanitatiza, mana kuna vitu humu mpaka najiuliza ni lugha gani hii.. please siku nyingine tunaomba lugha iwe ya kueleweka kwa faida ya sisi wakristo pia. Ahsante

 43. My brother recommended I might like this websitе.
  He used to Ƅe entirely right. This pսblіsh actually made my day.
  Уoᥙ can not believe simply how much time Ι һad spent for this info!
  Thanks!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s